Kansela wa Ujerumani asifu mazungumzo yake na Trump
6 Juni 2025Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz aliye ziarani nchini Marekani, amesema mkutano kati yake na mwenyeji wake Rais Donald Trump katika Ikulu ya Marekani ulikuwa mzuri na yenye tija. Merz ameelezea kwamba wamekubaliana na Rais Trump kuimarisha ushirikiano katika masuala ya biashara pamoja na masuala mengine.
Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya ziko mbioni kufikia makubaliano ya kibiashara kabla ya tarehe ya mwisho ya Julai 9 iliyowekwa na Trump kwa nchi 27 za Umoja wa Ulaya na washirika wengine wa kibiashara kwamba ziwe zimefikia mikataba ya kibiashara na Marekani kuepusha ongezeko la ushuru.
Ulaya, tayari inakabiliwa na ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa za chuma na alumini na ushuru wa asilimia 25 wa magari. Ulaya inaweza kukabiliwa na ushuru zaidi kwa mauzo mengine ya nje utakaongezeka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 50 iwapo hakutakuwa na makubaliano ifikapo Julai 9.