Kansela wa Ujerumani aapa kuuimarisha tena uchumi
14 Mei 2025Kansela mpya wa Ujerumani Friedrich Merz ameahidi leo Jumatano mageuzi na uwekezaji mkubwa wa uchumi kwa Ulaya baada ya miaka miwili ya mdororo wa kiuchumi.
Katika hotuba yake kuu ya kwanza bungeni, kiongozi huyo wa kihafidhina ameelezea msururu wa mipango kabambe ya kufufua uchumi unaosuasua hata kama unakabiliwa na tishio jipya la ushuru wa forodha wa Marekani.
Katika hatua nyingine Merz pia amegusia mpango wa Ujerumani kuwa na jeshi lenye nguvu zaidi barani Ulaya.
Soma pia: Kansela Merz amkaribisha Waziri Mkuu wa Ugiriki Mitsotakis
Merz "Katika siku zijazo, Serikali ya Shirikisho la Ujerumani itatoa rasilimali zote za kifedha ambazo jeshi la Ujerumani (Bundeswehr) inahitaji ili jeshi liwe kubwa na lenye nguvu zaidi. Hii inafaa kwa nchi ya Ulaya yenye watu wengi na yenye nguvu kiuchumi. Marafiki na washirika wetu pia wanatarajia hili kutoka kwetu, na kwa hakika wanatudai (tufanye hilo) kwa vitendo."
Merz na serikali yake mpya wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uchumi, ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi na miundombinu mibovu.