Kansela Schroader wa Ujerumani ziarani Saudi Arabia
28 Februari 2005Kansela Schroader alitahadharisha kwamba lengo la kibiashara la Ujerumani sio kuonesha ubwana, kwani wafanya biashara wa Kijerumani katika nchi za nje wanafanya mengi katika kuwapa mafunzo wafanya kazi vijana wa nchi hizo. Pia Kansela aliwataka wafanya biashara wa Ki-Saudia wawekeze zaidi katika Ujerumani, na hasa upande wa Mashariki ya Ujerumani ambako kuna miundo mbinu ya kisasa, nafasi nzuri kwa wawekezaji na wafanya kazi walio na ujuzi mzuri. Alisema hamu walio nayo wafanya biashara wa Kijerumani kwa Saudi Arabia ni kubwa kwa vile serekali ya Saudi Arabia imetekekleza marekebisho ya kuufungua na kuupanua uchumi wake. Aliihimza serekali ya ufalme huo iendelee na marekebisho hayo.
Mkuu huyo wa serekali ya Ujerumani alitoa mwito kwa Iran iwachane na mpango wake wa kinyukliya, na akasisitiza kwamba nchi hiyo isiwe na silaha za kinyukliya. Alisema mashariano baina ya Ujerumani, Uengereza na Ufaransa, kwa upande mmoja, na Iran , kwa upande mwengine, ya kutafuta suluhisho kwa mpango wa kinyukliya wa Iran ni ya kutia moyo. Na kwa mtizamo wake, utaratibu wa kutafuta suluhisho kwa mzozo wa Mashariki ya Kati umekuwa ni mwepesi zaidi. Kansela Schroader alisema, kama zilivyo nchi nyingine za Ulaya, Ujerumani iko tayari kushiriki kwa ukakamavu zaidi katika kutafuta suluhisho kwa ajili ya mzozo huo. Hiyo ni pamoja na kusaidia kuijenga mifumo ya usalama katika maeneo ya Wapalastina.
Kulitiwa saini mikataba kadhaa ya kibiashara yenye thamani ya mamilioni ya dola kati ya Ujerumani na Saudi Arabia, huku Kansela Schroader akishuhudia jambo hilo.
Kansela Schroader alitaja kwamba anakubaliana na Saudi Arabia kwamba uchaguzi uliofanyika huko Iraq ni hatua muhimu kuelekea kuifanya nchi hiyo kuwa ya kidimokrasia na kwamba Iraq ilio na amani na utulivu ni kwa maslahi ya watu wote. Alisema katika hali ya sasa ngumu inayojionea Iraq, Ujerumani iko tayari kuisaidia nchi hiyo. Ujerumani hivi sasa inawapa mafunzo wanajeshi na maafisa wa usalama wa Iraq katika Umoja wa Falme za Kiarabu na pia mafundi na wafanya kazi wa mikono wa Ki-Iraqi huko Kairo. Alitaja kwamba Ujerumani huenda karibuni ikajishughulisha yenyewe huko Iraq, punde hali ya usalama itakaporuhusu. Alisema punde pale hali ya usalama itakaporuhusu kutapelekwa wasaidizi wa Kijerumani wa kuijenga upya Iraq.
Jana Kansela Schroader alikutana kwa dakika tano tu na Mfalme Fahd wa Saudi Arabia katika Kasri lake. Mfalme huyo, mwenye umri wa miaka 83, kwa miaka sasa ni mgonjwa na shughuli zake za kiserekali zinaendeshwa na mrithi wa ufalme, mwana-mfalme Abdullah. Katika mazungumzo yaliofuata Kansela aliitia moyo serekali ya Saudi Arabia ifanye marekebisho zaidi ya kisiasa. Alisema mwenendo wa kuifungua nchi hiyo, bila ya shaka, ni wa tahadhari mno, na hauendi mbali mno, lakini ni maendeleo, hata hivyo. Katika duru za serekali ya Ujerumani imejulikana kwamba katika mazungumzo hayo ya jana pande zote mbili zilikubaliana kwamba Marekani ndio ilio na ufunguo wa mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati. Mrithi wa ufalme Abdullah aliitia moyo Ujerumani ijishughulishe zaidi katika ujenzi mpya wa maeneo ya Wapalastina.
Ufalme wa Saudi Arabia, ukiwacha Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mshirika muhimu kabisa wa kibiashara wa Ujerumani katika Ulimwengu wa Waarabu, lakini biashara hiyo inaonesha kupungua. Katika miaka 2003 na 2004, bidhaa zilizopelekwa na Ujerumani katika ufalme huo zilipungua kwa asilimia nane kila mwaka.
Katika kuyafungua maonyesho ya kuadhimisha miaka 75 ya mkataba wa urafiki baina ya Ujerumani na Saudi Arabia, Kansela Schroader aliwatia moyo vijana wa Saudi Arabia waje kusoma hapa Ujerumani na akatangaza kutatolewa misaada kwa wanafunzi kuwawezesha kutimiza jambo hilo. Katika hotuba yake ya kuyafungua maonyesho hayo alitoa mwito wa kuweko mdahala mkubwa zaidi wa kitamaduni baina ya nchi mbili. Alisema urafiki unakuweko pale watu wanapofahamiana na kuheshimiana na kwamba katika tamaduni zote kuna hamu ya kutaka kujuwa na kudadisi .
Leo mchana, Kansela Schroader anatazamiwa kuwasili Kuwait, ikiwa ni kituo cha pili cha ziara yake ya wiki moja katika nchi saba za Bara Arabu. Huko pia mazungumzo yatatwama juu ya masuala ya uchumi.
Miraji Othman