Kansela Merz amkaribisha Waziri Mkuu wa Ugiriki Mitsotakis
13 Mei 2025Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz, amemkaribisha Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, kwa heshima kamili za kijeshi mjini Berlin siku ya Jumanne. Mazungumzo yao yalijikita katika ushirikiano wa pande mbili, changamoto za bara Ulaya, na hali ya kisiasa duniani, huku suala la vita ya Ukraine likijitokeza kama kipaumbele cha haraka.
Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao, Merz alionya kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi ikiwa hakutakuwa na hatua madhubuti kuelekea amani wiki hii.
"Tunakubaliana kuwa ikiwa hakutakuwa na maendeleo halisi wiki hii, basi tutashirikiana katika ngazi ya Ulaya kuimarisha vikwazo kwa kiwango kikubwa," alisema Kansela huyo.
Merz alibainisha kuwa sekta ya nishati na masoko ya kifedha ni maeneo mengine yanayoweza kulengwa na vikwazo vipya. Kauli hiyo ilisisitiza mwelekeo mpya wa uongozi wake katika kuhimiza mshikamano wa Ulaya na kuishinikiza Urusi kumaliza uvamizi wake nchini Ukraine.
Soma pia: Ujerumani na Israel zaadhimisha miaka 60 ya uhusiano chini ya kivuli cha vita
Kwa upande wake, Mitsotakis alisisitiza kuwa Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa kiini cha juhudi za kusaka suluhu ya amani kwa Ukraine. "EU inapaswa kusimama pamoja," alisema, akionyesha uungaji mkono wake kwa msimamo wa Ujerumani.
Wakati wa ziara hiyo, viongozi hao wawili walionyesha mshikamano mpya kati ya mataifa yao mawili ambayo awali yalikuwa na misuguano, hasa wakati wa mgogoro wa madeni wa kanda ya euro na masuala ya uhamiaji. Lakini sasa wanaonekana kushirikiana kwa karibu ndani ya Umoja wa Ulaya.
Uchumi wa Ujerumani wazidi Kudorora, wito wa mazungumzo na Urusi waongezeka
Katika siku hiyo hiyo, Taasisi ya Kiuchumi ya Ujerumani (IW) ilikadiria kuwa uchumi wa taifa hilo utashuka kwa asilimia 0.2 mwaka 2025, na hivyo kuingia rasmi katika mdororo wa kiuchumi kwa mwaka wa tatu mfululizo. Sababu kuu zilitajwa kuwa migogoro ya kibiashara na Marekani, gharama kubwa za uendeshaji, na hali ya sintofahamu duniani.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Alexander Dobrindt, alitangaza marufuku dhidi ya kundi la mrengo mkali wa kulia, "Ufalme wa Ujerumani” (Königreich Deutschland), ambalo linatuhumiwa kuunda "dola mbadala” na miundombinu ya kiuhalifu.
Maafisa wa usalama walifanya msako katika majimbo saba na kuwakamata viongozi kadhaa wa kundi hilo, akiwemo mwanzilishi Peter Fitzek.
Katika hatua nyingine ya kidiplomasia, Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, ameitaka Urusi ichukue "hatua madhubuti” kwa kushiriki mazungumzo ya amani na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, yatakayofanyika wiki hii nchini Uturuki. "Urusi haipaswi kuacha kiti wazi ikiwa inamaanisha kweli amani,” alisema.
Soma pia: Trump na Ukuta na Reichsbürger Magazetini
Wakati Urusi bado haijakubali ombi la kusitisha mashambulizi mara moja, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, ametoa wito wa kuongezwa kwa msaada kwa Ukraine na kuongeza vikwazo dhidi ya Moscow, akisema Putin anaendelea na msimamo wake wa ukaidi.
Katika mlolongo wa matukio ya kisiasa, Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ameungana na mwenzake wa Israel, Isaac Herzog, katika safari ya kuelekea Israel kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili. Steinmeier ametaja urafiki kati ya mataifa hayo kuwa ni "muujiza wa kisiasa,” licha ya historia nzito ya Holocaust.
Kwa ujumla, Ujerumani chini ya uongozi mpya wa Friedrich Merz inaonyesha dhamira ya kuwa mhimili wa mshikamano barani Ulaya – ikiendeleza mazungumzo ya amani, kukabiliana na vitisho vya ndani kama siasa kali, na kutafuta njia mpya za kuinua uchumi uliodorora.