Kansela Merz aikosoa Israel kwa inachofanya Gaza
27 Mei 2025Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, ameikosoa vikali Israel kwa namna ambayo haijawahi kutokea, akisema mashambulizi ya anga yanayofanywa dhidi ya Gaza hayawezi tena kuhalalishwa kwa hoja ya kupambana na kundi laHamas.
"Imeonesha na inaonekana kwa mtazamo wangu kwamba muda umefika wa mimi kusema hadharani kwamba kile kinachotokea hivi sasa hakiwezi tena kukubalika na kwa hivyo tutaendelea na mazungumzo na serikali ya Israel.''
Kiongozi huyo wa Ujerumani, ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa nchini Finland ambako amekuwa kwenye ziara ya kukutana na viongozi wa nchi za kanda ya Nordic.
Ujerumani na Finland zimetowa mwito kwa mataifa ya ulimwengu kuishinikiza Israel kuruhusu misaada ya dharura ya kibinadamu kuingizwa Gaza.