Kanisa la Gwajima chini ya ulinzi mkali
3 Juni 2025vyombo vya ulinzi na usalama vilizingira kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima. Kanisa hilo limezingirwa ikiwa ni siku moja baada ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emanuel Kihampa, kulifungia kanisa hilo kwa madai ya kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa kwa nia ya kuichonganisha serikali na wananchi.
Hata hivyo, wakati usahihi wa barua hiyo ukiendelea kutafutwa, polisi walikwenda kulizingira kanisa hilo. Askofu Gwajima alirekodi video fupi na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii ikieleza hali ilivyokuwa katika kanisa hilo usiku wa jana:
"Ni saa tano na robo usiku, na hawa maaskofu unaowana wamekuja hapa usiku huu baada ya kusikia taharuki, Kwamba tunaona hapo polisi wamekuja kuzunguka kanisa la ufufuo na uzima, hapa Ubungo," alisema askofu Gwajima.
Tanzania : Bunge lawakalia kooni Gwajima na Silaa
Ingawa mpaka jana usiku Gwajima hakuthibitisha kupokea barua hiyo, lakini alisema wasaidizi wake walikuwa wamepokea barua ambayo alidai kutokuyasoma maudhui yaliyokuwamo ndani ya barua hiyo. Wakati hayo yakijiri, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amethibitisha polisi kuzingira kanisa hilo kwa madai ya kutekeleza sheria:
“Mtu ambaye amepewa mamlaka ya kisheria ya kusajili hizi taasisi za kidini, hicho kikiwa moja ya taasisi za kidini, alisitisha shughuli za taasisi za kidini inazofanya,” aliongeza kusema Muliro.
Kauli za Gwanjima zamuweka matatani
Haya yanajiri baada Askofu Gwajima ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kawe, Dar es Salaam, kupitia chama tawala cha CCM, kutoa kauli kwa nyakati tofauti akiishutumu serikali kwa matukio ya utekaji na upotevu wa watu.
Juzi katika ibada ya Jumapili iliyofanyika kwenye kanisa lake, Askofu huyo alisema yeye ni mwana CCM na CCM hakikubali utekaji.
Mjadala mzito Bungeni Tanzania kufuatia kauli ya Gwajima
Wakati hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, ameliambia Bunge asubuhi ya leo mjini Dodoma kwamba serikali itazihakiki taasisi za dini ambazo alidai zinafanya kazi kinyume na taratibu:
“Lakini ukifuatilia unakuta hajasailiwa, ukimgusa anasema serikali inavamia viongozi wa dini, kwa hiyo tunakwenda kufanya uchunguzi vizuri,” alisema Bashungwa
Juhudi za kumpata Askofu Gwajima kanisani kwake na kwa kutumia namba yake ya simu hazikuzaa matunda baada ya kuwepo taarifa zinazodai kuwa askofu huyo hajulikani alipo hadi tunakwenda hewani.