Kampala. Waasi wataka mashtaka dhidi yao yafutwe kwanza.
14 Septemba 2006Serikali ya Uganda na waasi wa Lord’s Resistance Army jana wamesisitiza misimamo tofauti juu ya kuondolewa kwa mashraka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kama sharti kuu kabla ya kupatikana makubaliano ya amani.
Mazungumzo yakiwa yamesitishwa hadi huenda wiki ijayo , serikali ya Uganda na waasi wa LRA wameimarisha misimamo yao juu ya iwapo mashtaka dhidi ya viongozi wa juu wa waasi yafutwe kabla ama baada ya kupatikana makubaliano.
Katika mjadala usio kuwa wa kawaida katika radio, kiongozi wa pili wa kundi la waasi wa LRA Vincent Otti na msemaji wa serikali Robert Kabushenga walijadili mada hiyo wakati wapatanishi wanatafuta njia za kupunguza mwanya baina ya pande hizo mbili ili kuruhusu majadiliano kuanza tena.
Akirudia madai ya hapo kabla , Otti amesema waasi wako tayari kutia saini makubaliano ya amani lakini hawatakubali kunyang’anywa silaha ama kurejea nchini Uganda hadi pale mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita itakapoondoa mashtaka yake dhidi yake binafsi na kiongozi wa kundi hilo Joseph Kony.