KAMPALA : Waasi waonywa kuwa watashambuliwa
20 Agosti 2006Uganda hapo jana imewaonya viongozi wa waasi wa LRA kwamba watashambuliwa kwenye maficho yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iwapo mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili yatashindwa.
Rais Yoweri Museveni amesema serikali ya Congo Kinshasa na serikali ya Sudan Kusini ambayo ndio mwenyeji wa mazungumzo hayo zimekubali mapendekezo ya serikali ya Uganda ya kufanya operesheni za kijeshi za pamoja dhidi ya waasi hao iwapo hakuna muafaka utakaofikiwa.
Amesema ikiwa mazungumzo hayo yatavunjika majeshi ya Uganda, Sudan ya Kusini,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na yale ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa yatamshambulia kiongozi mkuu wa LRA Joseph Kony na makamanda wake waandamizi ambao hivi sasa wamejichimbia katika Mbuga ya Taifa ya Garamba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Museveni akizungumza na waandishi wa habari kufuatia mkutano wake mjini Kampala na Makamo wa Rais wa Sudan Salva Kiir ambaye pia ni Rais wa Sudan ya Kusini amesema iwapo Kony haitumii fursa hii shambulio linamsubiri.