Kampala. Ujumbe wa Uganda waenda katika mkutano wa amani.
14 Julai 2006Serikali ya Uganda imesema jana kuwa itahudhuria mazungumzo ya amani nchini Sudan yenye lengo la kumaliza mapigano yaliyodumu kwa muda wa miongo miwili ya kundi la waasi la Lord’s Resistance Army , LRA, licha ya waasi hao kukataa kutuma viongozi wao wa ngazi ya juu.
Waziri wa mambo ya ndani wa Uganda, Ruhakana Rugunda, ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa majadiliano wa serikali, amesema kuwa kikosi chake kitaondoka leo Ijumaa kwenda katika mji wa kusini mwa Sudan wa Juba, ambako maafisa kutoka katika serikali ya eneo hilo lililo na mamlaka ya utawala wa ndani watafanya majadiliano ya upatanishi.
Haijafahamika hata hivyo iwapo majadiliano yataanza siku ya Ijumaa ama mkutano wa matayarisho utabidi kufanyika kwanza.