KAMPALA: Uganda kuchelewesha kutuma kikosi chake cha kulinda amani Somalia
4 Mei 2005Serikali ya Uganda imetangaza kwamba itachelewesha kutuma kikosi chake cha kulinda amani nchini Somalia. Tangazo hilo la Uganda limekuja siku moja baada ya kufanyika shambulio baya zaidi la bomu nchini Somalia ambapo watu kumi na tano waliuwawa wakati waziri mkuu wa nchi hiyo Ali Gedi alipokuwa akihutubia umma katika uwanja wa mpira nchini humo.
Uganda ilikuwa imepanga kutuma takriban kikosi cha wanajeshi 800 ifikiapo mwisho wa mwezi April ili kusaidia taifa hilo kuimarika upya.
Viongozi wapya wa serikali ya Somalia waliopo nchini Kenya wako chini ya shinikizo za kimataifa na wafadhili za kuwataka kurejea nyumbani licha ya nchi yao kukabiliwa na hali ya wasiwasi.
Hata hivyo rais Yoweri Museveni anatarajiwa kukutana na ujumbe wa mibabe wa kivita wa Somalia wiki hii ili kuijadili hali hiyo lakini wanasiasa wa Upinzani nchini Uganda wameikosoa hatua ya kutuma vikosi vyake katika nchi nyingine ilhali wanajeshi wangali wanakabiliwa na hali ngumu ya kupambana na waasi wa LRA nchini mwao.