Kampala. Obote kuzikwa rasmi kitaifa.
12 Oktoba 2005Uganda itafanya mazishi rasmi ya kitaifa kwa waziri wake wa kwanza na baadaye rais mara mbili , rais Milton Obote, ambaye amefariki dunia akiwa uhamishoni, licha ya madai kuwa anahusika na vifo vya watu zaidi ya laki tano.
Waziri wa habari wa Uganda James Nsaba Buturo amesema kuwa wameamua kuwa Bwana Obote anastahili mazishi ya kitaifa kama kiongozi mkuu wa kwanza wa serikali ambaye pia ameiongoza Uganda hadi kupata uhuru. Ameongeza kuwa Waganda wengi wanamuona Bwana Obote kama baba wa taifa , licha ya mauaji ambayo yalifanyika wakati wa utawala wake. Bwana Obote mwenye umri wa miaka 80, alifariki siku ya Jumatatu mchana mjini Johannesburg baada ya kulazwa Hospitalini kwa muda wa wiki kadha. Amekuwa akiishi uhamishoni nchini Zambia . Obote atazikwa katika kijiji alikozaliwa kaskazini ya Uganda katika tarehe ambayo haijatangazwa.