KAMPALA: Obote apata kikwazo cha kurudi Uganda.
8 Aprili 2005Serikali ya Uganda imemtaka Milton Obote kiongozi wa zamani wa taifa hilo aliye uhamishoni nchini Zambia kueleza jinsi watu wanaokisiwa laki tatu walivyo uwawa chini ya utawala wake kabla hajachukua hatua zozote za kutaka kurejea nchini Uganda.
Agizo hilo limefuatia ripoti kutoka kwa chama chake cha Uganda Peoples Congress UPC kuwa Milton Obote atarejea nchini Uganda mwezi ujao.
Waziri wa Habari na msemaji wa serikali ya Uganda Nsaba Buturo amemtaka Milton Obote kuwaeleza Waganda juu ya vifo hivyo kwanza kabla ya kurudi nchini.
Wakati wa utawala wa Obote kulitokea mauaji wakati wa mashambulizi baina ya serikali na waasi wakati huo wakiongozwa na rais wa sasa Yoweri Museveni.
Rais Museveni amesema kuwa serikali ya wakati huo ndio inayopaswa kulaumiwa kwa mauaji yaliyotokea.