KAMPALA : Mwili wa Obote wawasili Kampala
18 Oktoba 2005Mwili wa kiongozi wa kwanza wa Uganda huru Milton Obote umewasili nchini humo leo hii mchana baada ya kifo chake akiwa uhamishoni kubainisha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hasimu wake mkuu na Rais wa sasa wa Uganda Yoweri Museveni amepanda ndege na kuondoka nchini humo dakika chache kabla ya kuwasili kwa mwili wa Obote katika uwanja wa ndege wa Entebbe ukitokea Lusaka Zambia ambapo amekuwa akiishi uhamishoni kwa miaka 20.Haikuweza kufahamika mara moja iwapo kiongozi huyo atawahi kurudi kwa mazishi ya kitaifa hapo Jumapili kaskazini mwa Uganda.
Obote mwenye umri wa miaka 80 alikufa kutokana na ugonjwa wa figo katika hospitali ya Afrika Kusini hapo tarehe 10 Oktoba zaidi ya miongo miwili baada ya kun’golewa madarakani kwa mara ya pili na mapinduzi ya kijeshi.
Waganda wengi wanamsifu kwa mapambano yake ya kuwania uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Uingereza hapo mwaka 1962. Lakini wengine wanasema utawala wake hususan kwenye miaka ya mwisho mwisho ulikuwa umejaa dhila na ukatili wa kijeshi ambao umepelekea kuuwawa kwa takriban watu 300,000.