KAMPALA: Human right watch lashutumu makampuni ya magharibi kuchochea vita nchini Sudan-
25 Novemba 2003Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu " Human Right Watsch", linashutumu mashirika ya magharibi ya biashara ya petroli, kusababisha maafa makubwa katika zaidi ya miongo miwili iliyopita, nchini Sudan; kwa kuchochea vita.
Ripoti ya shirika hilo iliyotangazwa katika mji mkuu wa Uganda - Kampala, inashutumu miongoni mwa makampuni mengine, kampuni la Canada Talisman Energy, na kampuni la Swiden Lundin Oil, ingawa kutokana na shinikizo la mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu, makampuni hayo yamesitisha harakati zake katika maeneo ya kusini mwa Sudan, miaka miwili iliyopita.
Ripoti hio inasema asilimia sitini ya kitita cha dola za kimarekani miliyoni miatano themanini, zilizotokana na biashara ya mafuta ya petroli mwaka wa elfu mbili na moja, zilitumiwa na serikali ya Sudan, kununua zana za kijeshi.
Shirika la kutetea haki za binaadamu "Human Right Watsch" pia linashutumu waasi wa chama cha SPLA cha kusini mwa Sudan, kwamba wamekua wakiendesha vitendo vya kikatili na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, katika mapigano yaliyolenga kuteka maeneo yenye mafuta ya petroli. Shirika hilo linapendekeza raia wote wa maeneo ya kusini waliohamishwa kutoka makaazi yao kwa sababu ni maeneo yenye kua na mafuta, warejeshwe katika ardhi zao, au walipwe fidia, kama sehemu ya makubaliano ya amani yatakayosainiwa baina ya SPLA na serikali ya Karthoum.