Kambi kubwa za wakimbizi Kenya zakabiliwa na njaa
21 Julai 2025Maghala yako tupu, watoto wanaathirika kwa utapiamlo, na hospitali zimelemewa. Hii siyo baa la njaa ya ghafla – ni njaa ya taratibu, inayonyemelea kimya kimya.
Katika maghala ya Shirika la Chakula Duniani kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kilichobaki ni nafasi tu na mapipa matupu.
Akiba ya chakula imeshuka hadi asilimia 25 tu – na mbaazi kutoka Marekani ndizo bidhaa chache zilizosalia.
Tangu Februari, Marekani ilipositisha ufadhili wake, hakuna tena msaada wa chakula uliowasili.
Athari za hali hii zinamgusa moja kwa moja Regina Ngole, mama wa watoto saba kutoka Sudan Kusini. Akionyesha kikapu cha majani aliyovuna siku hiyo kwa familia yake, anasimulia hali ya maisha bila mgao wa chakula.
"Anaugua mara kwa mara. Hakuna chakula, na kwa sasa tunaishi kwa njaa." Alisema Regina Ngole, mkimbizi.
Mwezi Agosti, WFP inasema zaidi ya theluthi moja ya wakimbizi hawatapata chakula kabisa. Wale walio katika hatari zaidi wameahidiwa pesa kidogo kwa mwezi mmoja, lakini haitoshi.
Kwa wengi wanaoishi kambini – bila kazi wala vyanzo vya mapato – msaada huu wa chakula ndiyo njia pekee ya kuishi.
Watoto wakabiliwa na utapiamlo
Katika hospitali kuu ya Kakuma, hali imezidi kuwa mbaya. Watoto wengi wanaingia wakiwa na utapiamlo na kinga duni dhidi ya maradhi kama malaria na magonjwa ya tumbo.
Mwezi mbaya zaidi ulikuwa Machi, ambapo hospitali ilirekodi vifo vya watoto 15 – idadi isiyowahi kushuhudiwa.
Kefa Otieno, ni mkuu wa hospitali ya Kamati ya Uokoaji wa Kimataifa IRC, kambini hapo.
"Idadi kubwa zaidi ya vifo tulivyowahi kurekodi ilikuwa mwezi Machi – ambapo tulishuhudia vifo 15 katika wodi hii pekee, na hiyo ni dalili tu ya jinsi tulivyokumbwa bila maandalizi na ongezeko kubwa la wagonjwa tunaolazimika kuwahudumia hapa."
Picha na nembo za USAID bado ziko kila kona ya kambi, lakini misaada yao imekatika.
Shirika la WFP sasa linajiandaa kuwafahamisha wakimbizi kwamba hakuna chakula cha kutosha kwa wote.
"Huu ni mgogoro. Ni aina ya njaa inayoingia polepole, na hapa ndipo dunia inapaswa kutazama hali hii kwa umakini mkubwa na kurejesha ufadhili kwa shughuli za wakimbizi nchini Kenya." Alisema Colin Buleti, WFP Kakuma
Kwa sasa, kambi za Kakuma na Dadaab zimegeuka kuwa kioo cha ukimya wa dunia mbele ya janga la kibinadamu linalonyemelea – pole pole lakini kwa uhakika.