Kallas azungumzia uwezekano wa vikwazo vipya vya Urusi
15 Julai 2025Matangazo
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels Jumanne kujadiliana kuhusu kuiunga mkono Ukraine, miongoni mwa masuala mengine.
Mwezi Juni, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza awamu ya 18 ya vikwazo kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na hatua ya Rais Vladmir Putin kukataa makubaliano ya kusitisha mapigano.
"Bila shaka tuna matumaini kwamba makubaliano ya kisiasa yatafikiwa kuhusu awamu ya 18 ya vikwazo. Tuko karibu sana sana. Nina imani yatafikiwa leo," alifafanua Kallas.
Vikwazo hivyo vinalenga mauzo ya nishati ya Urusi pamoja na sekta yake ya benki na sekta ya kijeshi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo kwa njia ya video.