Kagame aionya Ubelgiji kwa kuichonganisha Afrika
17 Machi 2025Rais Kagame kwa mara nyingine tena ameilaumu Ubelgiji kuichonganisha Rwanda na mataifa mengine lakini akaahidi kuwa sasa yuko tayari kukabiliana na nchi hiyo ya Ulaya.
Rais Paul Kagame ameyasema hayo mjini Kigali katika ukumbi wa BK Arena ambapo zaidi ya watu elfu 8 walihudhuria tukio hilo. Hotuba hiyo ilirushwa moja kwa moja katika vyombo vyote maarufu vya habari na katika mitandao ya kijamii nchini Rwanda.
Rais Kagame amesema bila kigugumizi kwamba nchi ya Ubelgiji ambayo ni mkoloni wa zamani wa Rwanda na Kongo imekuwa mstari wa mbele kuyashawishi mataifa ya ulaya kuiwekea vikwazo Rwanda wakati nchi hiyo hiyo ya Ulaya ikiwa ndiyo kiini cha mzozo wa maziwa makuu tangu enzi za ukoloni
''Wabelgiji wameua raia wa Rwanda kwa miaka mingi zaidi ya historia hii ya miaka 30 mnayoijua, wametuua siku zote kila mara wanakwenda na kurudi, tumewaonya miaka mingi na sasa tunakwenda kuwaonya tena sasa.'' Alisema Kagame.
Mataifa makubwa ulimwenguni yanajiandaa kuiwekea vikwazo zaidi nchi ya Rwanda kwa shutuma za kulisaidia kundi la M23 linalopigana mashariki mwa Kongo, Rais Paul Kagame wa Rwanda amewatadhaharisha wananchi wake kuwa tayari kukabiliana na hali mbaya kutokana na vikwazo hivyo.
Soma pia:M23: Serikali ya DRC inahujumu mazungumzo ya Angola
Hotuba hii ambayo ilionekana kufafanua kiini cha mzozo wa mashariki mwa Kongo kwa wananchi imekuja wakati wimbi la vikwazo dhidi ya Rwanda kutoka mataifa makubwa likiendelea kurindima kutokana na shutuma kwamba Rwanda inalisaidia kundi la M23 ambalo linaendelea kuyateka maeneo makubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoka majeshi ya serikali.
Rais Kagame akizungumza kwa kuchanganya lugha za Kinyarwanda,kiingereza na Kiswahili amesema Ubelgiji ndiyo iko mstari wa mbele kuyahamasisha mataifa makubwa kuiwekea vikwazo Rwanda, akasema Ubelgiji na nchi nyingine za ulaya ndiyo zilipaswa kuwekewa vikwazo kutoka na kile yeye anasema ni nafasi yao katika kuliharibu eneo la maziwa makuu,
''Vikwazo baada ya vikwazo, hata wale ambao wanahusika na tatizo hili wao pia wanaomba vikwazo dhidi yetu, ni ajabu, kuna hata wakati mwingine unamuuliza mtu kwa nini mnataka kutuwekea vikwazo na kwa ajabu anajibu kuwa hajui kwa nini lakini kwamba anafanya hivyo kwa sababu Ubelgiji imewaomba wafanye hivyo.''
Vikwazo dhidi ya Rwanda
Nchi za ulaya, Marekani,na jumuiya ya nchi saba zinazoinukia kiuchumi ulimwenguni maarufu kama G7 zote zimeshatangaza kuwa zinajiandaa kuiwekea vikwazo Rwanda, lakini sasa miito na kauli hizo kutoka mataifa makubwa vinaonekana kumfanya Rais Paul Kagame kuwaandaa wanyarwanda dhidi ya athari zinazowasubiri ikiwa mvua ya vikwazo itaanza kunyesha kikamilifu
Rais Paul Kagame amelaani mataifa ya kigeni kufumbia macho serikali ya Kongo ambayo kwa kauli yake inaendelea kushirikiana na wanamgambo wa kihutu wa FDLR ambao wanafanya mauaji mchana kweupe dhidi ya raia wa Kitutsi mashariki mwa DRC huku jamii ya kimataifa ikifumba macho kama ilivyofanya nchini Rwanda mwaka 1994.
Soma pia:Angola yatoa wito wa kusitisha mapigano mashariki mwa Kongo
Taarifa za vikwazo zaidi dhidi Rwanda zimetangazwa sana baada ya nchi za jumuiya ya SADC kutangaza wiki iliyopita kwamba zitayandoa majeshi yake kutoka mashariki mwa Kongo hali ambayo ilifuatiwa na serikali ya Kinshasa kutangaza kuwa sasa imekubali mazungumzo na waasi wa M23 mjini Luanda Angola kesho Jumanne.
Hata hivyo haijulikani mstakabari wa mzozo huu wa Kongo kutokana na waasi wa M23 kuendelea hadi sasa kuyatwaa maeneo mengine licha ya serikali ya Kinshasa kukubali mazungumzo ya kuleta amani na mataifa makubwa kuendelea kuishinikiza Rwanda, je italeta suluhu? Ni kitendawili ambacho inasalia kazi kukitegua