Kabul:Bunge la Afghanistan kukutana
12 Desemba 2003Bunge la Afghanistan, Loya Jirga, Jumapili ijayo litaanza mdahalo wa katiba mpya ya nchi hiyo, miaka miwili baada ya Wataliban wenye sera kali kufukuzwa. Msemaji wa Kamati ya Katiba amesema kuwa tarehe iliyowekwa hapo kabla haikuweza kutekelezwa kwa sababu za kiufundi. Msingi wa mdahalo huo ni muswada utakaowasilishwa ambao utajadiliwa na Wabunge 500 na hatimaye kufungua njia ya uchaguzi wa kwanza ulio huru katika historia ya Afghanistan. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Lakhdar Brahimi, amesema kuwa matokeo ya mjadala utawategemea zaidi Wajumbe wa Baraza hilo. Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ujerumani, Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul, ametilia mkazo mjini Berlin kuwa anatumaini Loya Jirga litaweka msingi imara wa amani ya kudumu katika mustakabali wa Afghanistan.