KABUL: Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Peter Strück ziarani Afghanistan
29 Agosti 2005Waziri wa ulinzi wa Ujerumani bwana Peter Strück yumo nchini Afghanistan kuwatembelea wanajeshi zaidi ya 2,000 wa Ujerumani wanaolinda amani nchini humo, wakiwa ni sehemu ya kikosi kinachoongozwa na shirika la NATO.
Akizungumza na waandishi habari mjini Faizabad, waziri Struck amesema anatarajia mashambulio mengi zaidi kufanywa dhidi ya walinda amani kadri uchaguzi wa bunge unavyokaribia nchini humo.
Matamshi yake waziri Strück ameyafanya siku moja baada ya shambulio la roketi kufanywa katika kambi ya wanajeshi wa Ujerumani. Roketi hilo lilishindwa kuripuka kama ilivyotarajiwa na hakuna mwanajeshi aliyejeruhiwa katika hujuma hiyo.
Habari zaidi kutoka Kabul zinasema jeshi la Marekani linafanya kila liwezalo katika opareshini za kumsaka Osama bin Laden. Msemaji wa jeshi hilo, kanali James Yonts, amesema Marekani inashirikiana na mataifa jirani na Afghanistan, kama vile Pakistan lakini hakutaja ni wapi alikojificha kiongozi huyo wa kundi la al-Qaeda.