KABUL: Wapiganaji 8 wa taliban wauwawa nchini Afghanistan
8 Agosti 2005Matangazo
Wanajeshi wa Marekani na wa Afghanistan wamewaua wapiganaji wanane wa kundi la taliban katika mkoa wa Zabul, kusini mwa Afghanistan. Duru za jeshi zinasema wapiganaji wengine watatu wa kundi hilo wamekamatwa katika oparesheni hiyo iliyofanywa katika wilaya ya Shahr-i-Safa mkoani Zabul.
Msemaji wa taliban amesema wamewaua wanajeshi watatu wa Afghanistan na kuwateka nyara wengine 11 katika mkoa jirani wa Uruzgan. Mamia ya raia wamefariki dunia katika upinzani wa kundi la taliban unaolikumba eneo la kusini na mashariki mwa Afghanistan mwaka huu.
Ongezeko la machafuko hayo limesababishwa na kukaribia kwa uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, ambao kundi la taliban limeapa kuuvuruga.