KABUL: Uchaguzi wa Afghanistan wamalizika
18 Septemba 2005Tume ya uchaguzi nchini Afghanistan imetangaza kumalizika rasmi kwa uchaguzi uliofanyika leo nchini humo. Vituo vya kupigia kura vilifungwa mwendo wa saa kumi jioni kufuatia uchaguzi huo wa kwanza kuwahi kufanyika katika kipindi cha miaka 30 nchini humo.
Wapigaji kura walio katika mistari mirefu wakisubiri kupiga kura zao wataruhusiwa kufanya hivyo mpaka wamalizike.
Juhudi za wapiganaji wa kundi la Taliban nchini Afghanistan kuuvuruga uchaguzi huo hazikufua dafu hata licha ya kufanya mashambulio kadhaa katika eneo la kusini mashariki mwa nchi hiyo. Mfanyikazi mmoja raia wa Afghanistan alijeruhiwa vibaya wakati maroketi mawili yalipovurumishwa karibu na kituo cha kupigia kura katika ghala la umoja wa mataifa mjini Kabul.
Hapo awali askari polisi wawili na wapiganaji watatu walifariki dunia kufuatia mapigano makali karibu na mpaka wa Pakistan. Maofisa wamesema pia kwamba mpiganaji mmoja wa taliban aliuwawa katika mkoa wa Helmand, kusini mwa nchi hiyo wakati wapiganaji wengine walipofanya mashambulio dhidi ya kituo cha usalama mkoani Khost.
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai ameupongeza uchaguzi huo akisema nchi yake inataka kusahau miongo ya vita, misaada na mateso.