KABUL: Uchaguzi wa Afghanistan wakumbwa na machafuko
18 Septemba 2005Wapiganji wa kundi la Taliban nchini Afghanistan wamefanya mashambulio kadhaa katika eneo la kusini mashariki huku raia wengi wakijitokeza katika uchaguzi wa bunge na mikoa unaofanyika nchini humo hii leo.
Mfanyikazi mmoja raia wa Afghanistan amejeruhiwa vibaya baada ya maroketi mawili kuvurumishwa karibu na kituo cha kupigia kura katika ghala la umoja wa mataifa mjini Kabul.
Hapo awali askari polisi wawili na wapiganaji watatu walifariki dunia kufuatia mapigano makali karibu na mpaka wa Pakistan. Maofisa wamesema pia kwamba mpiganaji mmoja wa taliban aliuwawa usiku wa kuamkia leo katika mkoa wa Helmand, kusini mwa nchi hiyo wakati wapiganaji wengine walipofanya mashambulio dhidi ya kituo cha usalama mkoani Khost.
Uchaguzi huo ni wa kwanza kufanyika nchini humo katika kipindi cha miaka 30. Zaidi ya watu 1,000 wameuwawa katika mchafuko yaliyofanywa na kundi la Taliban, wakiwemo wagombea uchaguzi saba na mamia ya wapiganaji wa kundi hilo.
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai ameupongeza uchaguzi huo baada ya kupiga kura na kusema kwamba nchi yake inataka kusahau miongo ya vita, misaada na mateso.
Matokeo ya uchaguzi huo yatasaidia kuunda bunge na mabaraza ya mikoa huku taifa hilo likianza kuinuka tena tangu kuondolewa mamlakani kwa utawala wa Taliban kufuatia kampeni iliyoongozwa na Marekani mwaka wa 2001.