KABUL : Steinmeir ziarani Afghanistan
21 Agosti 2006Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeir ameanza ziara ya siku tatu nchini Afghanistan.
Ujerumani ambayo ina zaidi ya wanajeshi 2,800 waliowekwa nchini humo walichukuwa uongozi wa kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Usalama ambacho kilikuwa chini ya uongozi wa Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO huko kanda ya kaskazini miezi miwili iliopita.
Muda mfupi baada ya kuwasili katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul Steinmeir amewaambia waandishi wa habari kwamba Ujerumani imejizatiti kwa shughili za kulinda amani nchini humo kwa kipindi cha muda mrefu ujao.
Kuwasili kwa Steinmeir kunakuja katika siku ambayo imeshuhudia mapambano makubwa kati ya waasi wa kundi la Taliban na vikosi vya serikali ya Afghanistan na vile vya NATO kusini mwa nchi hiyo.
Zaidi ya wanamgambo 70 na wanajeshi watano wa Afghanistan wameuwawa katika mapambano kwenye jimbo la Kandahar.