Kabul. Rais wa Afghanistan ashutumu kuchomwa moto maiti za Wataliban.
22 Oktoba 2005Rais wa Afghanistan Hamid Karzai ameshutumu madai ya kitendo cha kuchoma moto maiti za wapiganaji wanaotuhumiwa kuwa ni wa Taliban kitendo kilichofanywa na wanajeshi wa Marekani.
Ametaka kufanyike uchunguzi wa haraka na Marekani kuhusu suala hilo. Ripoti iliyotangazwa na kituo cha televisheni cha Australia siku ya Jumatano imeonyesha picha za miili ya watu ikichomwa moto.
Wanajeshi hao wanadaiwa kuwa baadaye walitumia tukio hilo kuwatisha wapiganaji wengine.
Tukio hilo limeleta hasira kubwa miongoni mwa wananchi wa Afghanistan.
Uchomaji moto maiti ni haramu katika dini ya Kiislamu. Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Afghanistan wameonya kuhusu uwezekano wa kutokea hisia za kuipinga Marekani kutokana na tukio hilo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imesema kuwa tukio hilo haliakisi maadili ya Kimarekani.