Kabul. Polisi wawakamata watu kadha kutokana na kutekwa nyara kwa mwanamke mmoja mfanyakazi wa kutoa misaada.
17 Mei 2005Polisi wa Afghanistan wamewakamata watu kadha kuhusiana na kukamatwa mateka mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada raia wa Italia nchini humo. Maafisa wamesema kuwa Clementina Cantoni, ambaye anafanyakazi katika shirika la CARE International, alichukuliwa kutoka katika gari yake na watu wenye silaha katika mji mkuu Kabul jana Jumatatu.
Polisi wa Afghanistan wamesema wanaamini kuwa kundi la wahalifu, na sio wapiganaji wa Taliban ama al Qaida, linahusika na utekaji nyara huo. Hakuna kundi lililojitokeza kudai kuhusika na tukio hilo.
Wakati mji wa Kabul unaonekana kuwa uko salama zaidi kuliko mji mkuu wa Iraq Baghdad, wafanyakazi wa kutoa misaada wamekwisha toa onyo kwa wafanyakazi wao kutotembea ovyo kufuatia matukio mawili mengine ambayo hayakufanikiwa ya kuwateka nyara raia wa kigeni katika wiki chache zilizopita.