KABUL-Mfanyakazi wa kutoa misaada aliyetekwa nyara Afghanistan aoneshwa katika kituo binafsi cha Televisheni.
30 Mei 2005Kituo kimoja cha televisheni cha binafsi nchini Afghanistan,kimeonesha katika matangazo yake mkanda mfupi wa video unaomuonesha mfanyakazi wa shirika moja la kutoa misaada raia wa Italia aliyetekwa nyara siku 13 zilizopita.Katika mkanda huo anaonekana Clementina Cantoni mwenye umri wa miaka 32 akiwa amejifunika blanketi.Pia watu wawili wakiwa wamefunika nyuso zao,wanaonekana katika mkanda huo wakiwa wamemuelekezea mitutu ya bunduki kichwani mateka huyo wa Kitaliano.
Cantoni anayefanyakazi katika kituo cha kutoa misaada kinachojulikana CARE International,alichukuliwa kwa nguvu kutoka ndani ya gari lake na watu waliokuwa na bunduki tarehe 16 mwezi huu mjini Kabul.Bado haijajulikana watu hao waliomteka ni akina nani na pia madai yao hawajayaweka bayana.
Serikali ya Italia wameueleza mkanda huo wa video kama ni ishara ya uhakikishao na kuwa mazungumzo ya kuachiwa kwa Cantoni yanaendelea.