KABUL: Karzai akilaani kitendo cha kuchoma maiti za waasi wa taliban
22 Oktoba 2005Matangazo
Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai, amekilaani kitendo kilichofanywa na wanajeshi wa Marekani cha kuzichoma moto maiti za watu waliotuhumiwa kuwa wanamgambo wa kundi la taliban. Ametaka uchunguzi wa haraka ufanywe na Marekani kuhusu tukio hilo.
Picha zilizoonyeshwa katika televisheni nchini Australia ziliwaonyesha wanajeshi wa Marekani wakizichoma maiti hizo. Imedaiwa kwamba wanajeshi hao walikitumia kitendo hicho kuwatisha wapiganaji wengine wa kundi hilo.
Tukio hilo limezusha hasira miongoni mwa raia wa nchi hiyo, kwani dini ya kiislamu hairuhusu uchomaji wa maiti. Viongozi wa dini ya kiislamu nchini humo wameonya juu ya uwezekano wa kufanyika maandamano ya kuipinga Marekani na kuzuka kwa mashambulio.