Kabila amsuta Tshisekedi kuhusu mzozo mashariki mwa Kongo
24 Februari 2025Kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila amesema kuwa utawala mbaya wa mrithi wake, Rais Felix Tshisekedi, umechangia pakubwa katika kuzidisha mgogoro mashariki mwa nchi hiyo.
Soma: Tshisekedi amshutumu Kabila kwa kuunga mkono waasi
Kabila ameandika Makala ya maoni yaliyochapishwa kwenye gazeti la The Sunday Times la Afrika Kusini kwamba, mgogoro wa mashariki mwa Kongo hauwezi kulaumiwa tu kwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
Ameongeza kuwa uchaguzi wa Disemba 2023 uliompa ushindi Tshisekedi kwa muhula wa pili madarakani ulikumbwa na udanganyifu na kuilaumu serikali kwa kuzima sauti za upinzani.
Kabila ameendelea kueleza kwamba, tangu Tshisekedi achukue Madaraka mnamo mwaka 2019, hali nchini humo imezidi kuzorota hadi kufikia kiwango cha kile alichokiita, "karibu kusambarika kabisa.”