Kabila akutana na makundi ya wanawake Kongo
2 Juni 2025Kabila, ambaye anakabiliwa na tuhuma za kuwaunga mkono wapiganaji wa kundi la M23/AFC, alikutana na baadhi ya wanawake wanaoishi ndani na nje ya mji wa Goma. Hata hivyo, wanawake hao kutoka katika mashirika yakutetea haki za wanawake walitoa mwito wa kusitishwa kwa mapigano ili kuleta utulivu na usalama kwenye eneo hilo linalovuruga na vita.
Baada ya zaidi ya saa mbili za mazungumzo na rais huyo wa zamani aliyeliongoza taifa la Kongo kwa miaka 18 Kabla ya kumuachia usukani mrithi wake Felix Tshisekedi, bibi Bacho Tulinabo kiongozi na msemaji wa miungano ya wanawake mkoani kivu kaskazini, alilielezea ombi lao.
"Baada ya matatizo ya muda mrefu wanayoyapitia wanawake , tumemtaka rais wetu zamani kutuletea amani ,usalama pia kuanzishwa kwa shughuli za Benki ilikua ni kipaumbele katika mazungumzo yetu.Mbali na hayo tumemuomba pia afanye mazungumzo na rais wa sasa ili kupata suluhu kwa mzozo huu," alisema Bacho.
Aidha, wanawake hao ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wahanga wa matukio ya uhalifu yanavyofanywa na makundi ya waasi katika eneo la mashariki mwa Kongo, wametaka kupewa nafasi katika maamuzi yanayohusiana na amani, wakisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu kwa mafanikio ya mchakato mzima wa amani, alisema Liberata Buratwa, mama kutoka wilayani Rutshuru aliyeshiriki mkutano huo.
"Tafadhali, msimsahau mama katika mazungumzo sababu wanaume wanapigana lakikini wanawake huleta amani.watoto wote wanaokuwa porini ni sisi tuliowazaa, Rais ni sisi tuliye mzaa sababu gani tuendelee kuteswa.kwa hiyo ni vema kuwashirikisha wanawake wakati wa mazungumzo sababu ni mama ndiye mshauri mkuu iwapo ataketi pamoja na wanaume amani itapatikana," alisema Buratwa.
Katika ripoti yao ya mwezi Februari mwaka huu, wataalam wa Umoja wa Mataifa walieleza kusikitishwa kwao na ongezeko la matukio ya ubakaji yanayo kadiriwa kutokea kwa asilimia 94 kwa baadhi ya wanawake na wasichana wakati wa vita.
Kulingana na vyanzo vya ndani, Rais huyo wa zamani wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila ambaye aliyekuwepo kwenye makazi yake mjini Goma kwa siku kadhaa, ana nia yakuendeleza mashauriano ya amani na makundi yote ya kijamii na kisiasa kote katika eneo la Mashariki mwa Kongo.