KÖLON : Papa Benedikt ataka vijana kuacha kutumia dini watakavyo
21 Agosti 2005Papa Benedikt wa 16 amewatahadharisha vijana wa kikatoliki dhidi ya kutumia dini yao kwa kadri wapendavyo na kuiona kama bidhaa ya mlaji kwa kuchukuwa kile wanachokitaka na kupuuza sheria ambazo mara nyengine zinakuwa ngumu kutekelezwa.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 78 leo aliendesha misa katika sherehe za kufunga tamasha la Kanisa Katoliki la Siku ya Vijana Duniani katika mji wa Cologne Ujerumani.Ameutaka umma uliohudhuria misa hiyo kumeweka Mungu kwenye kitovu cha maisha yao na kusisitiza umuhimu wa kufanya ibada kila siku.
Watu wanaokadiriwa kufikia milioni moja walihudhuria misa hiyo kwenye uwanja mkubwa kabisa nje ya mji wa Kölon.Hilo lilikuwa ni tukio kuu la ziara ya siku nne ya Papa Benedikt katika nchi alikozaliwa na la kwanza tokea awe papa.Papa Benedikt ametangaza kwamba tamasha lijalo la Siku ya Vijana Duniani litafanyika Sydney nchini Australia hapo mwaka 2008.
Tamasha la Siku ya Vijana Duniani limeanzishwa na hayati Papa John Paul wa Pili.