Mzozo wa DRC: Jumuiya za EAC na SADC zatoa wito wa amani
8 Februari 2025Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki William Ruto, alifungua rasmi majadiliano hayo ya kuutafutia suluhu ya mgogoro huo kwa kutoa wito wa usitishwaji mara moja mapigano.
" Kuongezeka kwa uhasama hivi karibuni huko Goma na katika maeneo ya pembezoni, kuna-tukumbusha hali tete iliyopo sasa, na jambo la pekee tunalotakiwa kulifanya ni hatua ya pamoja ya kuwezesha kupatikana suluhu itakayoleta ahueni. Na sasa ndio wakati wa kuifanikisha hatua hiyo. Maisha ya mamilioni ya watu yanategemea uwezo wetu, hekima, busara na kutazama kwa undani jinsi ya kutatua changamoto hii kubwa, na kuyanusuru maisha ya mamilioni ya watu ambao wametumbukia katika sintofahamu na bila ya kuwa na uhakika."
Kwa upande wake, Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Emmerson Mnangagwa, amesema mkutano huo ni ushahidi wa dhamira ya jumuiya za EAC/SADC kwamba, juhudi zinaweza kuwezesha kuchukuliwa hatua za haraka ili kusitisha vita huko Kongo, huku akizitaka nchi za Afrika kushikamana kama ilivyokuwa wakati wa kutafuta uhuru kutoka kwa wakoloni.
Rais wa Rwanda ambaye nchi yake inatajwa kuwaunga mkono waasi wa M23 alishiriki moja kwa moja kwenye mkutano huo, huku rais wa Kongo Felix Tshisekedi akihudhuria kwa njia ya mtandao.