SADC kuondoa vikosi vyake mashariki mwa Kongo
13 Machi 2025Nchi 16 za jumuiya hiyo ya SADC zimechukua uamuzi huo leo baada ya kukamilika mkutano wa kilele kuhusu mzozo wa Mashariki mwa Kongo ambao umeshuhudia miongo mitatu ya machafuko na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu. Uamuzi huo unaeleza kuwa vikosi vya jumuiya hiyo vinavyofahamika kama SAMIDRC vitaanza kuondoka nchini Kongo kwa hatua kama alivyothibitisha Mwenyekiti wa SADC na rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.
" Mkutano huu maalum umepitisha uamuzi wa kijasiri wa kuondoa ujumbe wetu wa kulinda amani kutoka Mashariki mwa Kongo. Ni lazima tuharakishe utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa wakati wa mkutano wa pamoja wa SADC-EAC. Ikiwa ni pamoja na utekelezwaji wa michakato ya amani ya Rwanda na Nairobi. Zaidi ya hayo, mazungumzo ni msingi muhimu wa kuwahakikishia watu wa Kongo amani ya kudumu. Wakati ujumbe wetu ukiwa katika hatua ya kujiondoa, tunaomba ushirikiano wa kuwezesha hatua hiyo na ya kuhamisha vifaa vyetu."
Ujumbe wa SADC huko Kongo unaoundwa na wanajeshi kutoka mataifa ya Malawi, Tanzania na Afrika Kusini na ulitumwa mwezi Desemba mwaka 2023 kuisaidia serikali ya DRC, ambayo pia ni mwanachama wa SADC, kurejesha amani na usalama.
Tangu waasi wa M23 walipoazisha uvamizi wao na kuiteka miji ya Goma na Bukavu, Afrika Kusini ilipoteza mwezi Januari wanajeshi 14 kutoka kikosi cha SAMIDRC na wawili kutoka ujumbe tofauti wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Wanajeshi watatu wa Malawi pia waliuawa, huku Tanzania ikithibitisha vifo vya wanajeshi wake wawili.
Soma pia: Kwanini usitishaji vita Mashariki ya Kongo hauheshimiwi?
Afrika Kusini ndiyo iliyotuma idadi kubwa ya wanajeshi katika kikosi hicho ambao wanakadiriwa kufikia 1,000, lakini serikali ilikabiliwa na shinikizo la ndani la kutaka wanajeshi waliosalia huko Kongo waondolewe. Malawi mwezi Februari iliamuru jeshi lake kujiandaa na mchakato wa kujiondoa nchini humo.
Mazungumzo kati ya DRC na M23 kufanyika Angola
Uamuzi huu wa SADC unakuja siku moja baada ya Angola kutangaza kuwa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kongo na kundi la waasi wa M23 linaloungwa mkono na Rwanda yataanza wiki ijayo mnamo tarehe 18 Machi, 2025.
Soma pia: Wachambuzi watilia shaka uwezo wa vikosi vya SADC huko Congo
Licha ya watawala wa Kongo kukataa mara kadhaa kukaa meza moja na waasi hao ambao inawachukulia kama magaidi, baadhi ya vyanzo kutoka serikalni huko mjini Kinshasa vimeliambia shirika la habari la reuters kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo inafikiria kutuma wawakilishi kwenye mazungumzo ya amani huko nchini Angola. Taarifa ya mkutano huo imeidhinisha azma ya kuwepo suluhu la kisiasa na kidiplomasia katika mzozo huo na kuitaka jumuiya ya kimataifa kushughulikia mzozo wa kibinadamu unaoendelea kutanuka katika eneo hilo la Mashariki mwa Kongo.
(Vyanzo: AP, Reuters, AFP)